WAKAMATWA WAKIIBA SIMU MECHI YA SIMBA SC NA MWADUI FC IKIENDELEA...RPC ATAKA WALIOIBIWA WAKAZICHUKUE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia wanaume watatu kwa tuhuma za wizi wa simu za mkononi wakati mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Mwadui FC na Simba SC ikiendelea katika Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema wamewakamata watuhumiwa hao jana Jumapili Aprili 18, 2021 majira ya saa kumi jioni katika uwanja wa CCM Kambarage Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda Magiligimba amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Amos Shija (38) na Gerald Abdallah (18) wakazi wa Majengo pamoja na Rashid Hamis (25), mkazi wa Tabora watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Akielezea kuhusu tukio hilo, Kamanda Magiligimba amesema askari wakiwa katika majukumu ya kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa wakati wa Mechi ya Ligi Kuu kati ya Mwadui FC na Simba SC ikiendelea waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa wameiba simu tano.

“Tuliwakamata watuhumiwa wakiwa na simu tano ambazo ni Iphone 5 aina ya s7+ rangi nyeusi, Infinix hot 08, Sony xperia, Itel ndogo na Tecno rangi ya Silver”, amesema Kamanda Magiligimba.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga anaomba wananchi walioibiwa simu zao siku ya tarehe 18/4/2021 ndani ya uwanja wa CCM Kambarage kufika kituo kikubwa cha polisi Shinyanga ili kubaini simu zao.

Katika mechi hiyo, bao pekee la Nahodha John Raphael Bocco liliipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Mwadui FC kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Bocco alifunga bao hilo dakika ya 66 kwa kichwa akimalizia mpira uliounganishwa kwa kichwa pia na beki Mkenya, Joash Onyango kufuatia kona ya winga Mghana, Bernard Morrison kutoka upande wa kulia.

Ushindi huo unawafanya Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe pointi 52 baada ya kucheza mechi 22 na kurejea nafasi ya pili, sasa wakizidiwa pointi mbili na Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi tatu zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post