JAJI MSTAAFU DKT. BWANA AKERWA NA BAADHI YA WAAJIRI NA MAMLAKA ZA NIDHAMU KUTOFUATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (Kulia) akiteta jambo na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa Alhaj Yahya F. Mbila, leo Jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Tume kutoa uamuzi wa Rufaa na Malalamiko yaliyowasilishwa Tume na Watumishi wa Umma. (Picha na PSC).
Maafisa kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Maongezi, Katibu Msaidizi (kushoto), Bw. Ernest Mashiba, Afisa Sheria Mkuu (katikati) na Bw. Charles Mulamula, Mkurugenzi wa Sheria (kulia) wakishiriki katika Mkutano wa Tume unaotoa uamuzi wa Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma, mkutano unafanyika Jijini Dar es Salaam. 
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Khadija A. Mbarak (kushoto) na Kamishna Alhaj Yahya Mbila (kulia) wakishiriki katika Mkutano wa Tume unaofanyika Jijini Dar es Salaam kutoa uamuzi wa Rufaa na Malalamiko mbalimbali ya Watumishi wa Umma. (Picha na PSC).

*** 

Mwenyekiti  wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven James Bwana amewataka Viongozi walioteuliwa, wanaoteuliwa na kupewa dhamana ya Uongozi  kuwa wanapaswa kufahamu mambo ya msingi yanayohusu haki za watumishi ili wanapochukua hatua za kinidhamu watoe uamuzi wa haki.

Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana amesema haya Jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Umma unaoendelea kufanyika wa kupokea, kujadili na kutolea uamuzi rufaa na malalamiko mbalimbali ya watumishi wa umma yaliyowasilishwa Tume.

“Tunapojadili na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko mbalimbali yaliyopo mbele yetu tunabaini uwepo wa uzembe mkubwa unaofanywa na baadhi ya Waajiri na Mamlaka za Nidhamu wa kutokufuata Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kushughulikia masuala ya nidhamu ya watumishi walio chini yao. Kuna ucheleweshaji wa kuchukua hatua kwa baadhi ya Mamlaka hizi, kutokuchukua hatua stahiki kwa wakati kunaisababishia hasara Serikali” alisema Mheshimiwa Dkt. Bwana.

“Mtumishi wa umma anatuhumiwa kwa kosa la utoro kazini kwa zaidi ya siku tano bila ruhusa ya Mwajiri wake. Lakini baadhi ya Wajiri au Mamlaka za Nidhamu zinachukua hatua baada ya kipindi cha zaidi ya miaka miwili. Si sawa na huu ni uzembe mkubwa. Sheria imeelekeza hatua za kuchukua pale inapobainika mtumishi wa umma hayupo katika kituo chake cha kazi kwa zaidi ya siku tano bila ruhusa” alisema.

 

Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana alisema kuna umuhimu sana kwa Viongozi waliokwisha teuliwa na wanaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali katika Utumishi wa Umma kupatiwa mafunzo kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ili wafahamu mambo ya msingi ya kurejea wakati wa kutoa uamuzi wakati wanaposhughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa watumishi walio chini yao” alisema.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume, Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) John Haule amesema baadhi ya Mamlaka za Nidhamu zimekuwa zinachelewa kutekeleza maagizo ya Tume bila sababu ya msingi.

“Tume kupitia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa mbele yetu tumebaini udhaifu kwa baadhi ya Wakurugenzi na Mamlaka za Nidhamu wa kushindwa kutekeleza maagizo ya Tume. Mamlaka za Nidhamu zitekeleze maagizo ya Tume yanayotolewa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, kama hawakuridhika na uamuzi wetu wanayo nafasi ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais” alisema Mheshimiwa Haule.

 

Akizungumza katika mkutano huu Kamishna wa Tume, Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay, amesema Viongozi wanapaswa kuepuka kutenda ndivyo sivyo, wanapaswa kutenda haki kwa watumishi wanaowasimamia. Hii itapunguza malalamiko ya watumishi. Kwa watumishi wa umma, alisema wanapaswa kufahamu kuwa kutoa taarifa za uongo kwa mwajiri ni kosa.

“Watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia utoaji wa taarifa sahihi wakati wa kujaza fomu za  taarifa zao binafsi na fomu za Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS), wakidanganya au wakitoa  zisizo taarifa sahihi watachukuliwa  stahiki” alisema.

 

Mkutano wa Tume umeendelea leo tarehe 19 hadi 23 Aprili, 2021 ambapo rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma yaliyowasilishwa Tume yatatolewa uamuzi.

 

Imeandaliwa na:-

 

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

TUME YA UTUMISHI WA UMMA

19 Aprili, 2021

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post