TIMU ya Simba SC imekamilisha mechi zake za Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuchapwa 1-0 na wenyeji, Al Ahly usiku huu Uwanja wa WE Al-Ahly Jijini Cairo, Misri.
Bao pekee la Al Ahly limefungwa na Mohamed Sherif dakika ya 32 na kwa ushindi huo wanafikisha pointi 11, japo wanabaki nafasi ya pili wakizidiwa pointi mbili na vinara, Simba SC waliomaliza kileleni.
Ushindi huo ni sawa na mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa kulipa kisasi cha kuchapwa 1-0 pia kwenye mechi ya kwanza Februari 23, bao la Luis Miquissone Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Timu zote zimetinga Robo Fainali na Simba itakutana na ama Belouizdad ya Algeria kutoka Kundi B, Horoya ya Guinea Kundi C au MC Alger ya Algeria pia kutoka Kundi D, wakati Ahly itakutana na ama Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutoka Kundi B, Wydad Casablanca ya Morocco kutoka Kundi C na Esperance ya Tunisia kutoka Kundi D baada ya droo itakayopangwa Aprili 30 Jijini Cairo, Misri.
Chanzo - Binzubeiry
Social Plugin