Mwanamke aitwaye Happy Nyasumo (18) mkazi wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara amemuua mumewe, Bebe Mbogo (26) kwa madai kuwa hampendi na hakuwa chaguo lake zikiwa zimepita siku 14 tangu walipofunga ndoa.
Tukio hilo limetokea Aprili 14, 2021 saa 4 usiku katika kitongoji cha Pengo kijiji cha Iseresere ambapo inadaiwa chanzo ni mgogoro wa ndoa ambapo Happy alirudi kwao kwa madai kuwa hamtaki mumewe lakini huko kwao wakamlazimisha arudi kwa mumewe kwa maelezo kuwa hawawezi kurudisha ng'ombe waliochukua wakati wakimuozesha.
Diwani wa Majimoto, Johannes Masirori ambaye ni mjomba wa marehemu amesema Mbogo na Happy walifunga ndoa Machi 31, 2021 na kudai kuwa mwanamke huyo amekiri kufanya mauaji hayo.
"Kabla ya mauaji anadai kuwa mumewe alimlazimisha kufanya tendo la ndoa na baada ya kumaliza mwanaume alilala na yeye alipobaini amesinzia akachukua panga na kumkata mara tatu shingoni”,amesema.
Amesema baada ya kufanya kitendo hicho akiwa hana hofu Happy alikwenda kwenye nyumba ya mkwewe na kuchukua chakula na kuanza kula na kuwaonyesha panga alilokuwa ameficha na wakati watu wakilia na kusikitika kutokana na tukio hilo, Happy hakuwa na wasiwasi na aliwataka wasiojua wamtazame vizuri.
Social Plugin