Serikali imepiga marufuku matumizi ya malipo ya faini kwa kubeba fedha mikononi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Maganga amesema malipo yote yanayotokana na faini yanatakiwa kupitia kwenye mfumo rasmi ikiwemo kutolewa risiti za za kielektroniki (EFDs).
Naibu Waziri Maganga ametoa kauli hiyo leo Aprili 27, Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda aliyesema wananchi wanasumbuliwa hasa wanapokamatwa kuwa wameingiza mifugo kwenye hifadhi.
Katika swali la msingi Kakunda alitaka kujua ni kwa nini Serikali haitumii risiti za kielektroniki inapotoza faini za kuingiza mifugo kwenye hifadhi zilizopo Sikonge.
Naibu Waziri Maganga alisema kwa mujibu ya Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009, ni kosa kwa mtu yeyote (wakiwemo wafugaji) kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa.
Alisema Sheria hiyo haikuwekwa kwa ajili ya kujipatia mapato bali kudhibiti uharibifu ikiwemo uvamizi, ujangili na uingizaji wa mifugo ndani ya maeneo hayo kwa lengo la kuyatunza.
Maganga amesema Serikali imeanzisha mfumo wa Tehama kwa ajili ya utoaji wa leseni/vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato ya vyanzo mbalimbali vya sekta ya Maliasili na Utalii unaoitwa MNRT Portal ambao umefungamanishwa na Mfumo wa “Government electronic Payment Gateway - GePG” kwa ajili ya kutoa “Control Number” inayomwezesha mteja yeyote kulipa.
"Baada ya kufanya malipo husika mfumo wa MNRT Portal unatoa risiti ambazo zinatambulika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), napenda kumhakikishia Mbunge kuwa risiti zinazotolewa na mfumo huu ni halali kwa malipo ya Serikali sawa na zinazotolewa na mfumo wa Electronic Fiscal Devices (EFDs)," amesema Maganga.