Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera John Joseph
**
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kagera John Joseph, amesema wanamshikilia mkufunzi mmoja wa chuo cha Kilimo Maruku, kilichopo katika wilaya ya Bukoba kwa tuhuma za kumuomba rushwa ya ngono mwanachuo mmoja wa kike ambaye jina lake limehifadhiwa, ili amsaidie kufaulu mitihani yake.
Akizungumza na vyombo vya habari Joseph amesema kuwa mtuhumiwa huyo Ruta Cleophace Kyaragaine mwenye umri wa miaka 59 amekuwa akimtisha mwanachuo huyo kuwa asipomkubalia atamfelisha, hali iliyosababisha binti huyo kutoa taarifa kwa taasisi hiyo na mtuhumiwa kuwekewa mtego wa kukamatwa.
"Kufuatia kupokelewa kwa taarifa hiyo, tulianza kufanya uchunguzi na tarehe 03/04/2021 tulimkamata mkufunzi huyo akiwa katika nyumba ya kulala wageni iliyoko katika manispaa ya Bukoba jina linahifadhiwa, akiwa na mwanachuo huyo," amesema Joseph.
Wakizungumzia tatizo la uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono katika jamii, baadhi ya wananchi akiwamo Lydia Myaka wamesema kuwa kumrubuni mwanafunzi wa kike kufanya naye ngono ili asaidiwe katika mitihani ni dhambi na kuitaka serikali kuwachukulia hatua kali watakaobainika maana wanaharibu maisha yao.
Chanzo - EATV