Na Damian Masyenene, SHINYANGA
WAKATI Taifa na wanaharakati mbalimbali wakiendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, matukio ya udhalilishaji na ukatili kwa watoto yameendelea kuripotiwa mkoani Shinyanga, ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Juma Emmanuel (53) mkazi wa Nhelegani katika Manispaa ya Shinyanga kwa kosa la kubaka.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo Aprili 17, 2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 16, mwaka huu katika maeneo ya Ndembezi mjini Shinyanga, ambapo mtuhumiwa huyo alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 7 ambaye ni mjukuu wake.
Taarifa hiyo ya jeshi la polisi imeeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni mmonyonyoko wa maadili, ambapo mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo usiku kutoka chumba cha kulala watoto na kumpeleka kwenye chumba chake kisha kumuingilia kimwili.
“Mnamo Aprili 16, 2021 majira ya saa nne asubuhi jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga lilipokea taarifa kuwa maeneo ya Ndembezi, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 07 (jina linahifadhiwa) alibakwa na mtuhumiwa huyo ambaye ni babu yake….Mtuhumiwa alipata nafasi ya kufanya kitendo hicho wakati mke wake akiwa amelazwa hospitali kwa matibabu,” amesema Kamanda Magiligimba.
Amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, huku jeshi hilo likitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto vikomeshwe.