Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI KATAMBI: SERIKALI KUENDELEA KUWAPATIA VIJANA WA KITANZANIA MAFUNZO YA STADI ZA KAZI

Na: Mwandishi Wetu – Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa kuwapatia vijana ujuzi wa stadi za kazi na maarifa kama hatua mojawapo ya kuwawezesha vijana kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje.

Aliyasema hayo hii leo Aprili 20, 2021 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majiliwa (Mb) ambalo liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Latifa Khamis Juakali, ambaye alitaka kujua ni lini vijana wa Tanzania watapewa stadi mbalimbali za kuwaongezea ujuzi wa maarifa kupitia mfuko wa uwekezaji wa wananchi kiuchumi.

Akijibu swali hilo Mheshimwa Katambi, alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayolenga kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira.

“Jumla ya vijana 5,538 wamepatiwa Mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi katika nyanja mbalimbali kupitia Taasisi ya Don Bosco na Vyuo vilivyo chini ya VETA,” alieleza Katambi

Aliongeza kuwa, Serikali imeingia Mkataba na VETA wa kurasimisha ujuzi kwa vijana katika Mikoa yote nchini katika fani mbalimbali ikiwemo za Ufundi wa Magari, Useremala, Uashi, Upishi, Huduma za vyakula na vinywaji, Ufundi Umeme, Uchomeleaji vyuma, Ufundi bomba, Uchongaji Vipuri na Ushonaji wa Nguo.

“Katika mwaka wa fedha 2020/2021 kufikia Februari, 2021 jumla ya vijana 10,178 walikuwa wamerasimishwa na kati yao 28 ni Watu wenye Ulemavu,” alisema

Sambamba na hayo, alielezea Mafunzo ya Uzoefu Mahala pa Kazi ambayo yametoa fursa kwa Vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu kuendelea kuwashikiza kwa Waajiri ili kupata uzoefu makazini.

“Kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia Februari 2021, jumla ya wahitimu 1,203 wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati wamekamilisha mafunzo ya uzoefu kazini kupitia Viwanda, Taasisi na Kampuni mbalimbali za Sekta binafsi na Umma nchini na wahitimu 2,037 wanaendelea kupata ujuzi na uzoefu katika Taasisi binafsi na za umma na kati yao, wahitimu 92 ni Watu wenye Ulemavu,” alieleza Katambi

Aidha, Naibu Waziri Katambi alieleza vijana hao wanapomaliza mafunzo yao wamekuwa wakiwezeshwa kiuchumi kupitia mikopo yenye riba nafuu ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia halmashauri zilizopo nchini pamoja na Mfuko wa Maendeleo ambayo imekuwa chachu kwa vijana kuanzisha miradi mbalimbali.

Pia alibainisha kuwa serikali imekuwa ikitenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana katika halmashauri zilizopo nchini ili kuwasaidia vijana kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yanayowazunguka.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com