Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia mara baada ya kuwaapisha MAkatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumanne Aprili 6, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu amewataka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kujaza nafasi za walimu zaidi ya 6000 wanaohitajika kutokana na walimu hao wengine kustaafu na wengine kufariki na nafasi zao hazijazibwa tena.
Rais Samia ametoa kauli leo baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali ambao aliwateuwa Aprili 4, 2021, miongoni mwa viongozi hao ni makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa idara mbalimbali ambao amewataka wakachape kazi na kushughulika na mapungufu yaliyopo katika maeneo yao ya kazi.
“Kuna mahitaji ya Walimu zaidi ya 6000, Utumishi mpo hapa naomba muajiri hao walimu wakatoe huduma kwa Watanzania hivyo basi Tamisemi na Utumishi mkashughulike na hilo mara moja”, amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa, “Tamisemi mnajukumu kubwa la Elimu na Afya za Watanzania, mkasimamie miradi ya Elimu hasa Shule za Sekondari za Wasichana”.
Aidha Rais Samia ameongeza kuwa katika suala la ukusanyaji wa mapato,ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenda kukusanya mapato na matumizi yafanywe kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.