Katika kuadhimisha miaka 57 ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 5,001 waliokuwa wakitumikia adhabu ya vifungo mbalimbali.
Kati ya wafungwa hao, 1,516 wameachiwa huru baada ya kupunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini ya kifungu cha sheria ya Magereza sura ya 58.
Wafungwa wengine 3,485 wamepunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini yakifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa wafungwa 3,485 waliopunguziwa adhabu zao wataendelea kutumikia sehemu ya kifungo iliyobaki.
Kupitia taarifa hiyo, Rais Samia amewataka wafungwa wote walioachiwa huru kutumia vyema mafunzo walyopata wakiwa gerezani na waungane na wanachi wenzao katika ujenzi wa taifa huku wakiheshimu na kuzingatia sheria za Taifa.