Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini viashiria vya ubadhilifu wa fedha kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendesha Tamasha la ‘Urithi Wetu’ kinyume na kanuni husika.
Akizungumza leo jijini Dodoma, CAG Charles Kichere amesema fedha zilizotumika kufanikisha tamasha hilo, hazikuwa katika bajeti ya wizara hiyo, wala hakukuwa na mpango ulioidhinishwa wa utekelezaji wake.
Amesema kutokana na fedha hizo kuwa nje ya bajeti, wizara hiyo ilichangisha kiasi cha shilinigi bilioni moja kutoka katika wakala zake nne ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wanyapori Tanzania (TAWA).
“Kila moja ilitakiwa kuchangia shilingi milioni 250 ambazo hazikuwa kwenye bajeti zao, ili kuwezesha kufanyika kwa tamasha hilo,” amesema
Amesema ili kuongeza bajeti hiyo, wizara ilichangia shilinig bilioni 299 na Mfuko wa Fedha za Maendeleo ya Utalii shilinig bilioini 270 na jumla ya shilingi bilioni 1.57 zilipatikana ili kufanikisha utekelezaji wa tamasha hilo.
CAG Kichere amesema amebaini hakukuwa na stakabadhi zinazothibitisha malipo ya shilingi milioni 831.1 kutoka kwa wizara hiyo kwenda kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa ajili ya maonyesho ya kulitangaza tamasha hilo.
“Hata hivyo, hakukuwa na risiti za kielekroniki kuthibitisha kupokelewa kwa malipo hayo na hao waliolipwa,” amesema CAG
Amesema kodi ya zuio kiasi cha shilingi milioni 41 hazikukatwa katika malipo yaliyofanyika.
“Aidha, kodi ya zuio ya Shilingi milioni 31 na shilingi milioni 10 kutoka Clouds TV na TBC mtawalia haikukatwa katika malipo yaliyofanywa.” alisema na kuongeza
“Wizara haikupata hizo kodi ya zuio. Ushaidi unaonesha kuwa, manunuzi ya huduma za matangazo kwa TBC na Clouds, zilipatikana kwa njia ya ushindani usiosawa,” alisema