Wizara ya Nchi Ofisi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/22 inatarajia kuajiri watumishi wa umma wapya 44, 096.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 22, 2021 Waziri wa wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa, wakati akiwasilishwa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Mchengerwa amesema kada ya elimu wataajiri watumishi wapya 10,297, afya 11,215, kilimo 1,383, mifugo 1,250, uvuvi 733, Jeshi la Polisi 1,782, Magereza 843, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji 512 na watumishi wapya wa hospitali za mashirika ya kidini na hiari 1,240.
Ameongeza kuwa serikali itaajiri watumishi 14,841 wa kada mbalimbali ikiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu vyote vya umma nchini pamoja na kada nyingine ambazo haziko kwenye sekta zilizoainishwa awali.
Hata hivyo, amesema watumishi 92,619 wa kada mbalimbali watapandishwa vyeo na watumishi 2,360 watabadilishwa kada katika utumishi.
Amebainisha kuwa maelekezo yatakayotolewa wakati huo ni kuchambua na kuhakiki madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma 17,699 yenye thamani ya Sh37.47 bilioni na kuchukua hatua ipasavyo.