Na Alex Sonna,Dar es Salaam
Mabingwa wa Tanzania timu ya Simba imetinga hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa mabao 4-1 As Vita Club kutoka Kongo na kufikisha Pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na Al Ahly ya Misri Mchezo uliopigwa uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba walikuwa wa Kwanza kuliona lango la wageni kupitia kwa winga machachari Luis Miquissone dakika ya 30 kwa shuti kali akipokea pasi kutoka kwa Bernard Morisson ,mnamo dakika ya 32 kiungo Zemanga Soze akasawazisha na kuvunja rekodi ya Simba ya kutoruhusu bao.
Kabla ya Mapumziko Simba walipata bao la pili kupitia kwa kiungo Mshambuliaji Clatous Chama dakika ya 45 na kuipeleka Simba mapumziko ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko hata hivyo Simba ilinufaika na mabadiliko hayo akitokea benchi Larry Bwalya aliipatia Simba bao la tatu akimalizia pasi ya Clatous Chama dakika ya 66.
Mnamo dakika ya 83 Clatous Chama alirudi tena kambani kwa bao safi kwa kuwachambua mabeki wa As Vita pamoja na golikipa wao mara baada ya kupokea pasi ya Luis Miquissone.
Kwa ushindi huo Simba wamefikisha Pointi 13 na kuongoza kundi A ambapo hawawezi kufikiwa na timu yoyote baada ya Vibonde Al-Merreikh kuwakazia Al Ahly kwa kufungana mabao 2-2 ,Simba wamebakiza mechi moja ugenini dhidi ya Al Ahly ambao wana pointi 8 hata kama Simba atapoteza bado ataongoza kundi A.
As Vita na Al-Merreikh rasmi wameshindwa kuendelea hatua ya robo Fainali na kuwachia Simba na Al Ahly wakisonga mbele ya Michuano hiyo Mikubwa barani Afrika.
CHANZO - FULLSHANGWE BLOG