TANZANIA YAWAHAKIKISHIA MAZINGIRA MAZURI WAWEKEZAJI WA MAREKANI


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani mazingira mazuri na kuwasihi kuendelea kuwekeza hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Donald Wright katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema makampuni mbalimbali kutoka Marekani yameonesha nia ya kuwekeza katika sekta za nishati, miundombinu, afya na kilimo hususani katika zao la korosho.

“Katika kikao changu na Balozi tumejadili na kusisitiza umuhimu wa Kampuni za Marekani kuwekeza nchini Tanzania.........na Balozi amenihakikishia baadhi ya kampuni hizo zipo tayari kuwekeza hapa nchini,” amesema Balozi Mulamula

Aidha, Mhe. Waziri Mulamula amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania kujipanga kutumia fursa ya kuuza Marekani bidhaa mbalimbali zinazozalishwa hapa nchini.

Kwa Upande wake Balozi wa Marekani, Mhe. Wright amesema uhusiano wa Marekani na Tanzania ni wa miaka mingi na kuahidi kuuendeleza na kuimarisha uhusiano huo.

“Suala la wawekezaji kuja kuwekeza hapa Tanzania nimemhakikishia Mhe. Waziri kuwa suala la wafanyabishara na wawekezaji wa Kimarekani kuja kuwekeza hapa Tanzania ni jambo ambalo nimelipa kipaumbele na ninalifanyia kazi kwa karibu ili wawekezaji wa Kimarekani waendelee kuja kuwekeza kwa wingi Tanzania,” amesema Balozi Wright

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mulamula amekutana kwa maongezi na Balozi wa Comoro hapa nchini, Mhe. Dr. Ahmada El Badasui pamoja na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić ambapo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano.

“Tumekubaliana kukutana na tume za ushirikiano ili tuweze kujadili na kuona ni jinsi gani tunaweza kuboresha masuala ya biashara na ushirikiano katika maeneo mbalimbali,” amesema Waziri Mulamula.

Nae Balozi wa Comoro hapa nchini amesema nchi yake  itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha uhusiano huo unaendelea kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Leo nimepokelewa na Waziri Mulamula na tumejadiliana masuala ya ushirikiano baina ya Comoro na Tanzania na pia tumeongelea masuala mbalimbali yanayohusu mabalozi hapa Tanzania pamoja na maeneo ambayo tutaanza kuyafanyia kazi kati ya Comoro na Tanzania,” amesema Mhe.  El Badasui.  

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Milišić amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafanikisha malengo ya maendeleo endelevu iliyojiwekea katika kuwaletea maendeleo watanzania.

“UN itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inafanikisha agenda zake za maendeleo endelevu,” amesema Bw. MiliÅ¡ić.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post