TIC YARIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA SARUJI CHA TANGA CEMENT JIJINI TANGA

Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda wa pili kulia akisisitiza jambo kwa  Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema leo wakati walipotembelea na kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanywa na Kiwanda cha Saruji cha Tanga Cement kilichopo Jijini Tanga kulia ni Nestory Kissima na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha fedha kwenye kiwanda hicho Issac Lupokela

 

Mkuu wa Kitengo cha fedha wa Kiwanda cha  cha Tanga Cement,Isaac Lupokela akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo katikati ni Mhandisi Benedict Lema akifuatiwa na
Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda na Nestory Kissima
Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema akizungumza jambo wakati wa ziara hiyo
Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo
Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda
Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo kulia ni Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda

MENEJA wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda leo ametembelea na kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanywa na Kiwanda cha Saruji cha Tanga Cement kilichopo Jijini Tanga huku akieleza kuridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na kampuni hiyo kwa kuchangia kiasi kibwa katika maendeleo ya nchi.

Meneja huyo wa TIC,Daudi Riganda amefanya ziara leo Jumatatu Aprili 19,2021 akiwa ameambatana na Nestory Kissima.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali kwenye kiwanda hicho, Bw. Riganda alisema mwekezaji wa Kampuni ya Tanga Cement ni miongoni mwa wawekezaji mahiri waliosajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania na kupewa hadhi ya wawekezaji mahiri.

Bw. Riganda alisema wamefika kiwandani hapo kuangalia uwekezaji uliofanyika na kuangalia mkataba “Performance Contract” uliosainiwa baina ya Serikali na Wawekezaji hawa ni namna gani ulivyotekelezwa na kila upande. 

 

Katika ziara hii, TIC wamejionea uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 147.65 uliofanywa na kampuni hii, huku ajira zipatazo 330 za moja kwa moja na 677 zisizo za moja kwa moja zikitengenezwa kupitia uwekezaji huu. Kampuni ya Tanga Cement ni miongoni mwa makampuni yanayoongoza katika kulipa kodi katika Kanda ya Kaskazini. 

Aidha Alisema imeonekana kwamba kuna matokeo makubwa yaliyopatikana upande wa teknolojia ambazo zimeingizwa nchini kupitia mradi huo huku akieleza kufurahishwa zaidi na namna kampuni hiyo ilivyofanikiwa kuajiri idadi ndogo ya wafanyakazi wa kigeni huku idadi kubwa ikiwa ni wafanyakazi wa Kitanzania, wengi wao wakiwa ni vijana wa kitanzania.

“Wapo wafanyakazi wa kigeni hawazidi watano na idadi kubwa walioajiriwa kwenye mradi huu wakiwa  ni vijana wa Kitanzania kwa hakika hili limetufurahisha sana",alisema

Meneja huyo alisema suala lingine ambalo limewafurahisha ni jinsi suala la mazingira na usalama kazini yalivyozingatiwa kuanzia unapoingia getini mpaka unapotoka kiwandani.

Hata hivyo, imebainika kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake kupitia mkataba walioingia na wawekezaji hawa hasa katika kipengele cha msamaha wa kodi ya zuio “withholding tax” kwenye mkopo wa kigeni ulioingizwa na kampuni hiyo kutoka nchini Afrika ya Kusini kwa vile serikali ilipaswa kutoa notisi kwenye Gazeti la Serikali kuruhusu msamaha huo kitu ambacho hadi hii leo hakijafanyika.

Kutokana na dosari hii maafisa wa TRA waliwaandikia kuwataka kulipa kodi yote kama inavyopaswa na pale walipotoa maelezo walijikuta wakifungiwa akaunti zao za benki, kitu kilichowafanya kuanza kulipia kodi hiyo.

Bw. Riganda aliahidi kufuatilia suala hilo ili kuhakikisha mamlaka za serikali zenye dhamana ya kuhakikisha mikataba inayoingiwa baina ya Serikali na wawekezaji inasimamiwa kama ilivyosainiwa.

Meneja huyo alisema wao kama Kituo cha Uwekezaji watawasilisha malalamiko hayo kwa mamlaka za serikali kupitia Mkurugenzi wao wa kituo cha Uwekezaji ambaye atazungumza na Waziri wa Uwekezaji ndani ya ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia namna gani mikataba hiyo baina ya wawekezaji mahiri na serikali inaheshimika ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kuwapata wawekezaji nchini.

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema alisema huo ni mradi mpya wa laini ya kuzalisha Clinka uliogharamu kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 147 na walisaini mkataba huo na TIC.

"Lakini mpaka sasa haijatangazwa na Gazeti la Serikali na hivyo  kuifanya Serikali kuonekana haijatimiza wajibu wake kulingana na mkataba ulioingiwa na pande hizo mbili, kitu kilichosababisha usumbufu kwa wawekezaji hasa kwenye masuala ya kodi ambazo TRA inawadai”, alisema.

Kampuni ya Tanga Cement ilikuwa na mpango wa kufungua kiwanda kingine cha saruji mkoani Arusha jirani na eneo la uwanja wa ndege wa KIA, mradi ambao ulikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 50,hata hivyo wawekezaji hao wamesitisha mpango huo ambao ungetengeneza ajira na mapato zaidi kwa serikali, hadi hapo suala hili la kimkataba “performance contract” litakapopata suluhisho na kodi hiyo kusamehewa kama ilivyobainishwa kwenye mkataba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post