WAZIRI JAFO AAGIZA VIBALI VYA UKUSANYAJI, USAFIRISHAJI NA UHIFADHI WA CHUMA CHAKAVU VITOLEWE KWA MIAKA MITATU


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Suleiman Jafo ametoa agizo kuwa vibali vyote vya ukusanyaji, usafirishaji na uhifadhi wa vyuma chakavu vitolewe kwa muda wa miaka mitatu na sio kwa mwaka mmoja kama ilivyokua awali ili kuepusha usumbufu kwa Wawekezaji. Ametoa agizo hilo alipokuwa katika ukaguzi kwenye  kiwanda cha Metro  steel Ltd kinachozalisha nondo kilichopo Kiwalani jijini Dar es Salaam.

Aidha akiwa katika kiwanda hicho pia Mh. Jafo ametoa onyo kwa wenye viwanda kwa kutokufuata sheria, taratibu na kanuni za mazingira. Pia alitoa rai kwa wenye viwanda kwa kulinda miundombinu ya Nchi na  kutokufanya uharibifu katika kupata vyuma chakavu.

Ameendelea kusema kiwanda hicho cha Metro Steel Ltd  kinalalamikiwa na wananchi kuwa muda wa usiku kinatoa moshi na kupelekea kero kwa wakazi walio karibu na kiwanda.

“Natoa onyo kali kwa kiwanda hiki leo sijaja kupiga faini ningeweza kumwambia Mkurugenzi Mkuu wa NEMC awapige faini ila ninawapa onyo  mjirekebishe katika hili”. Alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt.  Samuel Gwamaka amesema kiwanda cha Metro steel kina kibali cha usafirishaji lakini kibali hakina tarehe wala kiasi cha chuma chakavu kilichosafirishwa na kushushwa kiwandani. “Utaratibu uliopo lazima kibali kiandikwe tarehe na kiasi cha chuma chakavu kinachosafirishwa na vinginevyo kutoandikwa tarehe kibali kimoja kinaweza kutumika bila kikomo hivyo kuwa na kibali kisichoandikwa tarehe ni makosa”. Dkt. Gwamaka

Katika ziara hiyo pia Waziri Jafo alifanya ziara alitembelea kiwanda cha Steel Masters kukagua uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kutoka katika chuma  chakavu. Akiwa katika kiwanda hicho pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa laHifadhi na  Usimamizi wa Mazingira (NEMC),Dkt. Samwel Gwamaka, walikagua lori lenye usajili T620 AQW likiwa na bidhaa mbalimbali za chuma likingojea kushusha mzigo ambapo walijiridhisha kuwa lori hilo linakidhi mahitaji yote ya kisheria yanayotakiwa.

Waziri Jafo amefanya ziara katika viwanda viwili katika jiji la Dar es Salaam ikiwa ni ziara yake ya kukagua masuala ya mazingira katika viwanda hivyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post