VIJANA 854 WA JKT WALIOANDAMANA KWENDA IKULU WATIMULIWA
Sunday, April 18, 2021
Mkuu wa majeshi nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema vijana 854 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini wamesitishiwa mikataba yao na kurudishwa majumbani.
Mabeyo ameeleza hayo jana Jumamosi Aprili 17, 2021 katika hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mjini Dodoma.
"Aprili 8, 2021 vijana wetu wa JKT wapatao 854 walianzisha mgomo, kukataa kufanya kazi maeneo mengine na kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa madai ya kutaka kumuona rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa rais wa Tanzania, John Magufuli."
"Vijana hao ni kati ya vijana 2400 walioahidiwa kuandikishwa jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya kazi katika maeneo mengine lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa jeshini, " amesema Mabeyo.
Amebainisha kuwa jeshi halikuwa na lengo hilo na limelazimika kusitisha mikataba yao kwa kuwa kosa walilolifanya ni sawa na uasi na hauvumiliki.
Ameeleza kuwa pamoja na kufanya uchunguzi wa kwa nini walifanya hivyo, jeshi limeamua kutafakari upya mpango wa kuchukua vijana wa kujitolea kwa ajili ya kujiunga na JKT.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin