Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAAJIRI ZINGATIENI MASLAHI YA WATUMISHI WA UMMA


 Na. Veronica Mwafisi-Mtwara
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutoa kipaumbele kwenye maslahi ya watumishi, ikiwa ni pamoja kuwaasa Maafisa Utumishi kufanya ufuatiliaji ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata stahili zao kwa wakati.   

Mheshimiwa Ndejembi ametoa wito huo kwa Waajiri na Maafisa Utumishi akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa hiyo.

Akitoa mfano wa uzembe wa Afisa Utumishi mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mhe. Ndejembi amesema afisa huyo amesababisha watumishi wapatao 236 kutopata stahili ya kupandishwa madaraja kwa kisingizio cha kuchoka jambo ambalo halikubaliki katika Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, kitendo cha kutowapandisha madaraja watumishi hao kwa wakati kimewanyima haki yao ya msingi kwani katika Utumishi watalazimika kutengewa upya bajeti katika mwaka wa fedha mwingine ili waweze kupandishwa madaraja kwa mujibu wa sifa za miundo ya kada zao, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uadilifu na utendaji kazi wao.

Sanjali na hilo, ameelezea kitendo cha waliokuwa Watumishi wa Umma katika Halimashuri ya Wilaya ya Kibaha ambao mpaka wanastaafu mwaka jana hawakupandishwa madaraja kwa wakati jambo ambalo limeathiri mafao yao.

Kutokana na changamoto ya watumishi hao kutopata stahili, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitomvumilia mwajiri au Afisa Utumishi yeyote atakayesababisha Watumishi wa Umma kutopata masilahi au stahili zao kwa wakati.

“Tukibaini kuna Mwajiri au Afisa Utumishi yeyote anayezembea na kusababisha watumishi waliopo kwenye taasisi yake kukosa stahili zao kwa wakati, Serikali haitomvumilia kwani atakuwa anaharibu taswira nzuri ya ofisi yake ikiwa ni pamoja na taswira ya Mhe. Rais ambaye amehimiza Watumishi katika Taasisi zote za kupata stahili zao.

Kwa niaba ya Viongozi na Wakuu wa Idara waliopo katika Taasisi za Umma mkoani Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mhe. Seleman Mzee amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwahimiza kutekeleza majukumu yao kikamilifu hususani suala la uzingatiaji wa masilahi ya Watumishi wa Umma mkoani Mtwara.

Mhe. Mzee ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyowapewa na Mhe. Ndejembi mara watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi na kuongeza kuwa, watatoa kipaumbele kwenye suala la masilahi ya Watumishi wa Umma ili kuwajengea watumishi ari ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kutoa huduma bora kwa umma.

Mhe. Ndejembi, amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika Taasisi za Umma mkoani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com