Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Kahama, Abdallah Urari
Na Salvatory Ntandu - Kahama
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imefanikiwa kumkamata Majaliwa Kayaya Isanduko mkazi wa mtaa wa Nyakato akiwa na nyama za nguruwe waliokufa akiziuza katika duka lake la nyama huku ikielezwa kuwa nyama hizo pia huuzwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.
Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 21,2021 na Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Kahama, Abdallah Urari wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo na kusema kuwa Majaliwa alikamatwa na taasisi hiyo baada ya kupokea taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuwa anajihusisha na uuzaji wa nyama za nguruwe waliokufa.
Alisema kuwa baada ya taarifa hizo walianza ufuatiliaji kwa kushirikiana na maafisa mifugo na ambapo aprili 13 mwaka huu walifanikiwa kumkamata na nyama za nguruwe ambazo katika mahojiano yetu alikiri kuchinja na kuuza nyama za nguruwe waliokufa katika duka lake huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria..
“Majaliwa alitozwa faini baada ya kukamatwa kwa makosa mawili kosa la kwanza ni kuchinja nguruwe bila kibali amelipa shilingi laki mbili na kosa la pili ni la kuuza nyama (Vibudu) amelipa shilingi laki mbili. Faini hizi ni kwa mujibu wa sheria za mifugo zinazosimamiwa na manispaa ya Kahama,”alisema Urari.
Sambamba na hilo Urari alisema kuwa katika uchunguzi walioufanya walibaini kufukuliwa kwa nyama za nguruwe zilizofukiwa na maafisa mifugo wa halmashauri hiyo baada ya kubainika kuwa na kasoro katika eneo la Nyakato wakati wa usiku na kuingizwa sokoni kinyemela hali ambayo inaweza kuhatarisha afya za watumiaji wa kitoweo hicho.
“TAKUKURU imeagiza kufungwa kwa machinjio yote bubu ya nguruwe wilayani Kahama na kumwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, kuhakikisha anatenga eneo maalum la machinjio haraka ili wafugaji wote wa nguruwe waweze kupeleka mifugo yao kwa ajili ya kuchinjwa. Tusipochukua hatua za haraka inaweza kuhatarisha usalama wa afya za watumiaji wa kitoweo hicho kutokana na watu kuendelea kula mizoga,”aliongeza Urari.
Alisema kuwa nyama hizo zinazofukuliwa baada ya kuzikwa ardhini na maafisa mifugo baada ya kubaini kuwa na kasoro na hazifai kuliwa, zimekuwa zikifukuliwa na kuuzwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji jambo ambalo ni hatari kwa afya za walaji na wananchi wanapaswa kuwafichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Social Plugin