WAZIRI GWAGIMA APIGA MARUFUKU AKINA MAMA KUUZIWA KADI ZA KLINIKI


Na.WAMJW-Morogoro
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima   amepiga  marufuku utaratibu wa kuwauzia kadi za kliniki akina mama wajawazito pamoja na zile za watoto baada ya kuzaliwa wanapopelekwa kliniki za chanjo  kwani ni kinyume  na mwongozo wa serikali.

Dkt. Gwajima Aliyasema hayo jana mjini Morogoro alipokuwa akiongea na timu ya wataalamu wa afya halmashauri na mkoa huo kwenye kikao cha kujadili changamoto za afya ya uzazi, mama na mtoto.

"Nimekua nikipokea malalamiko mengi toka sehemu mbalimbali ya nchi kwamba mama mjamzito au mama akijifungua kadi ya kiliniki wanauziwa kutoka vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, hii hapana". Alisema

Hata hivyo Waziri huyo alisema amebaini ni kweli kadi hizo zinauzwa Jambo ambalo siyo maelekezo ya serikali bali ni utaratibu binafsi wa  baadhi ya viongozi wa afya na watumishi wasio na mapenzi mema kwa serikali na wananchi.

Aidha, alisema kufanya hivyo ni kukosa  ubunifu na uwezo katika kukabiliana na changamoto za kawaida kabisa mahala pa kazi na hivyo kuwataka watumishi hao kutatua changamoto hiyo kwani gharama za kupata kadi hizo ziko ndani ya uwezo wa halmashauri kitu ambacho wanaweza kuondoa uhaba huo katika maeneo yao bila kusubiri .

Alizitaka pia  halmashauri zote nchini kuanzia leo kupata ufumbuzi wa ukosefu wa kadi hizo na asisikie tena malalamiko kutoka kwa akina mama wanaofika kliniki kwani Serikali haitaki kuwaona akina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano wanapata shida hizo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post