Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AWATOA WASIWASI WATANZANIA KUHUSU MFUMO WA KUYAENDELEZA MAKAO MAKUU YA NCHI DODOMA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatoa hofu Watanzania kuhusu kuendelezwa kwa Makao Makuu ya nchi Dodoma kwa kuwaeleza kwamba Serikali imeweka mfumo mzuri utakaohakikisha yanajengwa kuendana na mipango ya maendeleo ya Jiji la Dodoma.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Aprili 16, 2021) wakati akihitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

Amesema mfumo huo, unahusisha Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ambacho kinajumuisha wajumbe kutoka Wizara na Taasisi za Serikali. “Kikosi Kazi hicho kina jukumu la kushauri namna bora ya kupanga na kuendeleza Mji wa Serikali na Jiji la Dodoma kwa ujumla”.

Waziri Mkuu amesema utekelezaji huo, unahusisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji, kiwanja cha ndege, barabara na utoaji wa huduma za jamii. “Niwahakikishie Watanzania wote kuwa Dodoma inaendelea kujengwa”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wabunge na Watanzania warejee kauli ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa waendelee kushikamana, kusimama na kuwa wamoja kama taifa, kuoneshana upendo na undugu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu, utanzania wetu na kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini.

“Huu si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele. Kwa msingi huo, tuendelee kudumisha na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili. Tutumie muda mwingi kwa kazi zaidi za kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja.”

Vilevile, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulioanza katikati ya wiki hii. “Nitoe rai kwamba tutumie kipindi hiki kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake”.

“Kadhalika, tumuombe Mwenyezi Mungu awajalie viongozi wetu hekima na busara ili waendelee kuliongoza Taifa letu kwa haki, kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani katika nchi yetu pamoja na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com