Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati alipofika mkoani hapo kwa ajili ya kufungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania utakaofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare. (21.04.2020)
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu Mifugo kwenye mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania ambapo wamewataka wafugaji kuhakikisha wanasimamia na kuyatunza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.
Baadhi ya Viongozi na wajumbe wa mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania wakisikiliza Hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akimkabidhi Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Rogers Shengoto (kulia) Kitabu cha Mpango Mkakati wa Kwanza wa Utekelezaji wa Malengo ya Chama cha Malisho Tanzania wa Miaka Mitano 2021-2025 kwenye mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji kusimamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na kuhakikisha wanayatunza.
Ndaki ameyasema hayo (21.04.2021) wakati akifungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Edema katika mkoani Morogoro.
Wafugaji wametakiwa kuhakikisha wanayasimamia na wanayatunza maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kuyaendeleza kwa kupanda malisho na kuweka miundombinu ya maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo yao.
“Ni lazima maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji tunayalinda na kuyaendeleza kwa kupanda malisho na kuweka miundombinu ya maji na siyo kuyaacha yabaki kama mapori kwani watumiaji wengine wa ardhi wanaweza kuanza kuyatumia na baadae migogoro inaanza,” alisema Ndaki.
Ndaki pia amewataka wafugaji kuhakikisha wanaendelea kuomba ardhi kwa ajili ya shughuli za ufugaji katika vijiji na kumilikishwa kwa kupata hati za kimila ili waweze kuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao lakini pia waweze kupanda malisho.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri Ndaki amesema viongozi ni lazima wabadili fikra pale wanapoona mifugo imeingia katika maeneo yao, badala ya kulalamika inatakiwa watafute suluhisho kwani uwepo wa mifugo ni fursa kiuchumi katika maeneo yao.
Vilevile amewataka wataalam kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi na upandaji wa malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Ndaki amekishukuru Chama cha Nyanda za Malisho Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanyana na amewahakikishia kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuwapa ushirikiano kwani malisho kwa mifugo ni jambo la muhimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare amesema kuwa mkoa wake kwa asilimia kubwa una wafugaji na wakulima lakini tatizo kubwa lililopo ni watu kupata ardhi bila kufuata utaratibu, hata kwenye maeneo ambayo tayari yalishapimwa na kutengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na watumiaji wengine wa ardhi.
Sanare amesema kwa sasa wanaendelea kuwadhibiti watu ambao wanavamia ardhi bila kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi kwenye vijiji na wataalam ambao wametoa hati za kimila bila kufuata utaratibu au kwa kutojiridhisha.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema wizara imekuwa ikishirikiana na Chama cha Nyanda za Malisho na wataalam katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya uendelezaji nyanda za malisho hapa nchini.
Dkt. Rwiguza amesema wameshirikiana na chama hicho katika maandalizi ya Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho ambapo mwongozo huo upo katika hatua za mwisho ili uweze kuwasilishwa kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni yao.
Wizara kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Chama cha Nyanda za Malisho imeendelea kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi inayowahusu wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Vilevile Dkt. Rwiguza amewasihi wafugaji kuhakikisha wanayatumia Mabaraza ya Ardhi ya Kata pale wanapokuwa na migogoro ya ardhi.
Mwenyekiti wa Chama cha Nyanda za Malisho Tanzania, Dkt. Ismail Selemani amemshukuru Waziri kwa kukubali mwaliko wao na kushiriki katika kikao hicho. Lakini pia amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kila mwaka imekuwa ikiendele kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na Nyanda za Malisho.
Dkt. Selemani amesema kupitia wizara wanashuhudia kasi ya uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mifugo na mazao yake hali ambayo itasaidia kukuza uchumi wa wafugaji na kuongeza mchango wa mifugo katika pato la taifa.