Nteghenjwa Hosseah, Tanga
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Uongozi wa Jiji kuona namna watakavyoongeza kujenga sehemu ya michezo ya watoto katika Jengo la Kitega Uchumi linaloendelea kujengwa Maeneo ya Kange Jijini hapo.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Jengo la Kitenga Uchumi linalojengwa katika eneo la Kange Jijini Tanga kukagua maendeleo ya mradi huo tarehe 26.04.2021
Waziri Ummy alisema kuwa Tanga hakuna maeneo mazuri ya michezo ya watoto kwahiyo ni wakati sasa Jiji la Tanga kuangalia namna mnavyoweza kujenga maeneo hayo ili kuwapa fursa watoto wetu kucheza na kufurahi katika Jiji lao.
Aidha Mhe. Ummy Mwalimu(Mb) ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi linaloendelea kujengwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Akizungumza katika mradi huo amesema Jengo hilo likikamilika sio tu kwamba litapendezesha mji lakini pia litakua chanzo cha mapato kwa Jiji la Tanga.
“Mradi huu ni wa mfano kwa Halmashauri zingine kuiga na kuanza kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato ya Halmashauri zao” aliongeza Waziri Ummy.
Pia aliwataka Uongozi wa Jiji la Tanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na thamani ya fedha inaonekana.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Maeji alisema kuwa Mradi huo wa Kimkakati ni Jengo la Gorofa moja litakua na huduma za Kibenki, migahawa, maduka, supermarket na maduka ya vinywaji na maeneo ya mama lishe.
Maeji aliongeza kuwa mradi huo mpaka kukamilika utagharimu shilingi Bilioni 8 na utakamilika Nov,2021.