AWESO : ZINGATIENI UHALISIA, HATUTAKI BILI KICHEFUCHEFU ZA KUUMIZA WANANCHI


Na Mohamed Saif
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amezitaka Mamlaka za Maji kote nchini kuacha mara moja kuwapa malengo ya makusanyo yasiyo na uhalisia wasomamita wake ili kuepuka ankara (bili) bambikizi.

Aweso ameelekeza hayo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya siku moja kwenye ujenzi wa miradi ya maji kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela Mkoani Mwanza ili kujiridhisha na hatua iliyofikiwa.

“Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchi nzima ninawapa salam mzifikishe kwa Mameneja Biashara wenu, waelezeni waache mara moja kuwapa wasomamita wao malengo yasiyo na uhalisia,” alielekeza Waziri Aweso.

Alisema ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji lakini pia ni wajibu kwa mwananchi huyo anayepokea huduma kulipa ankara yake lakini isiwe ya kubambikizwa.

“Leo unampa malengo makubwa msomamita ambayo hawezi kuyakusanya na hivyo anachoweza kufanya ni kumbakizia mwananchi wa kawaida ili tu kukufurahisha wewe bosi wake,” alisisitiza Waziri Aweso.

Alisema ni vyema Mamlaka za Maji zikaweka makadirio yenye uhalisia juu ya ukusanyaji wa mapato kwa maana bili za maji ili kila mwananchi aweze kulipia.

Waziri Aweso alionya kuwa Serikali haitovumilia Mamlaka ya Maji inayowaumiza wananchi kwa kuwabambikizia wananchi usomaji wa mita  usiostahili. “Msiruhusu wasomamita wawaletee usomaji usiokuwa na uhalisia, hakikisheni mnajiridhisha vyakutosha kabla hamjamtumia ankara mwananchi,” alielekeza,

Hata hivyo alisisitiza kuhusu wajibu wa mwananchi anayepokea huduma wa kuhakikisha analipa ankara yake kwa wakati ili kusaidia jitihada za Serikali kuboresha  na kupanua wigo wa utoaji wa huduma hususan kwenye maeneo yenye changamoto.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji endelevu na toshelevu na hivyo ni muhimu kila mmoja wetu akatimiza wajibu wake ili kufikia lengo hilo,” alielekeza Waziri Aweso.

Aidha, katika ziara hiyo, Waziri Aweso ameelekeza wakandarasi kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwamba Serikali haitotoa muda wa nyongeza kwa Mkandarasi yoyote atakayeshindwa kukamilisha mradi kwa muda uliyopangwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post