Misheck Nyandoro (66) muumini wa Kanisa la Johanne Marange Apostolic ambaye ni baba wa watoto 151 kutoka kwa wake 16 amesema hatakoma kuzaa.
Nyandoro kutoka Mbire, eneo la Kati mwa Mashonaland nchini Zimbabwe, alisema alioa mke wa kwanza mwaka 1983 na alipumzika kuoa kwa muda mwaka 2015 lakini sasa ana mpango wa kuoa mke wa 17 ili amzalie watoto wengine zaidi, Gazeti la The Herald limeripoti.
Kulingana na mzee huyo aliyezaliwa mwaka 1955 na kujiunga na Kanisa la Johanne Marange Apostolic mwaka 1972 ndoa ya mitaala ni mradi ambao aliuanzisha mwaka 1983 na ataendela nao hadi kifo.
"Yangu ni mradi. Huu mradi wa ndoa ya mitala niliuanzisha tangu mwaka 1983 na nitaumaliza na kifo changu. Wakati nitafariki ndio nitakoma kuoa na kuzaa watoto. “Ninapanga kuoa mke wangu wa 17 msimu huu wa baridi na tayari mipango inashughulikiwa," alisema Nyandoro.
Kulingana na mzee huyo mwenye umri wa miaka 66, mradi huo unazaa matunda kwani hupokea pesa na zawadi nyingi kutoka kwa watoto wake na wakwe.
“Kutokea kwa watoto wangu wanaofanya kazi na kuzawadiwa pesa kupitia EcoCash, karibu kila siku, watoto wangu 11 wameniweka kwenye sera ya mazishi.
Ninapata zawadi kutoka kwa wakaza wanangu (wakwe zangu)." “Sijakoma kuzaa wala kuoa. Mungu akiniruhusu, nitaoa hadi wake 100 na huenda kuzaa watoto 1000. Ulaya una mpango wa kupunguza idadi ya watu Afrika na ninapinga.Mimi ni mpiganaji wa kitambo na serikali inashuhulikia katro ya watoto wangu. Hakuna shida," aliongeza.
Mzee huyo amesema watoto wake 50 bado wanasoma shule,sita wameajiriwa Jeshini,wawili ni askari polisi, wengine 11 wameajiriwa maeneo mbalimbali,mabinti zake 13 wameolewa, vijana wake 23 wameoa mmoja wao akifuata nyayo za baba yake ameoa wake wanne na wake zake wawili sasa wana ujauzito.
Nyandoro alifichua kuwa kazi yake ni kuketi kwenye kivuli na kusubiri chakula kutoka kwa wake zake 16 ambapo kila mke hupika na yeye huchagua tu chakula kitamu na kutupa kilichopikwa vibaya akidai ni sheria katika boma hilo.
Mzee huyo alijigamba namna ana uwezo wa kuwaridhisha wake zake chumbani ambapo ana ratiba ya kumtembelea kila mke kuwapa haki zao za ndoa.