MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewaomba wakazi wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo wamchague Dkt. Florence Samizi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa ndiye atakayewaletea maendeleo.
“Uchaguzi hauhitaji ushabiki wala mbwembwe bali umakini mkubwa ili kumpata kiongozi atakayekuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia na kuwasemea mahali popote naye si mwingine ni Dkt. Florence Samizi. Tumchague Dkt. Florence hakuna kitakachoharibika.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo Jumanne, Mei 4, 2021 alipozungumza na wakazi wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Taifa, Kibondo Mjini.
Amesema wakimchagua Dkt. Florence watarahisisha shughuli za maendeleo katika jimbo hilo zikiwemo za ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama ya afya, barabara. “Wana-Muhambwe wote twende na Dkt. Florence Samizi kwa maendeleo ya Muhambwe”.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha hospitali ya wilaya ya Kibondo ili kuhakikisha wakazi wa wilaya hiyo wanapata huduma bora za afya.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo, hivyo wamchague Dkt. Florence kwa kuwa ndiye atakayeweza kusimia miradi hiyo.
“Mchagueni mgombea kutoka CCM kwa sababu ndicho Chama kinachowahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote. CCM inawahudumia wananchi bila kujali uwezo wake wa kifedha, bila kujali ukabila. Tumchague Dkt. Samizi atuletee maendeleo.”
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Augustino Vuma amewaomba wakazi wa jimbo la Muhambwe wamchague Dkt. Florence kwa sababu ni kiongozi mnyenyekevu, msikivu na ndiye atakayeweza kushirikiana nao katika kutatua changamato zinazowakabili.