Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RPC MAGILIGIMBA AONYA WAVUNJIFU WA AMANI SIKUKUU YA EID EL-FITR SHINYANGA….ASHUKURU WADAU KWA USHIRIKIANO


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba
***

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

 Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limewataka wananchi  wote kuwa makini katika kusherehekea  Sikukuu ya Eid-El-Fitr kwa amani na utulivu kwa kujiepusha na vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari Mei 12,2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora amesema uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi cha Sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya Uhalifu kutokana na mikusanyiko ya watu.

“Ikumbukwe kuwa, Wananchi wenye imani ya Kiislam na hata madhehebu mengine huutumia muda wa Sikukuu kwenda kuabudu  pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe.

Napenda kuwaondoa hofu wananchi wote kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote mkoani hapa wanasherehekea Sikukuu kwa Amani na Utulivu kwani Ulinzi umeimarishwa maeneo yote ya Ibada, Mabwawa ya Kuogelea (Swimming Pool), sehemu za Kumbi za Starehe na Burudani, pamoja na maeneo mengine yote ya wazi yatakayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu”,amesema Kamanda Magiligimba.

Amewatahadharisha watumiaji wote wa barabara kuwa makini kwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani  na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.

“Napenda kusisitiza zaidi juu ya kuimarisha Usalama kwenye Kumbi za Starehe kwa kuwaasa wamiliki wa kumbi hizo kuhakikisha wanazingatia uhalali wa matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu, umri unaostahili na zaidi kujali uwezo wa ukumbi husika. Tabia za kimazoea zikiwemo zile za kuendekeza tamaa za kifedha na kujaza watu ukumbini kupita kiasi pamoja na disco toto ni marufuku na hatua kali za kisheria zitachukuliwa mara moja kwa yeyote atakayethubutu kufanya hivyo”,ameeleza.

Pia amewaasa na kuwasisitiza Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla kuendelea kuwa makini zaidi na uangalizi wa watoto wao, watoto wa majirani na watoto wa jamii kwa ujumla, waepuke kuwaacha wakitembea peke yao au wakati mwingine kuzurura barabarani na maeneo mengine ili kuepuka ajali na maafa au matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara kwa watoto wetu.

 

“Nitoe wito kwa wananchi watakaolazimika kutoka katika makazi yao kwenda katika ibada au kwenda katika sehemu mbalimbali za starehe, wahakikishe kuwa hawaziachi Nyumba/makazi yao wazi au pasipo uangalizi na watoe taarifa kwa majirani zao, niwasisitize wananchi wote kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mapema pale watakapowatilia mashaka watu wasiowafahamu/wanaowafahamu kuwa wahalifu pindi watakapowabaini katika maeneo yao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo”,ameongeza. 

“Nitumie fursa hii muhimu kuwatakia wananchi wote Mkoa wa Shinyanga, SikuKuu njema ya Eid-El-Fitr kwa kuwahakikishia kuwa Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa, pamoja na Miongozo mbalimbali inayotolewa mara kwa mara. Hivyo, halitawajibika kumwonea muhali, huruma ama Upendeleo mtu yeyote atakeyekwenda kinyume na Sheria”,amesema Kamanda Magiligimba.

Kamanda huyo wa polisi ametumia fursa hiyo kuwashukuru Wananchi wote, Vyama vya Siasa, Makampuni Binafsi ya Ulinzi, Kamati ya Usalama Mkoa Shinyanga, Kamati za Usalama Wilaya zote, Taasisi mbalimbali za Serikali, Madhehebu ya Dini, Asasi za kiraia na Wanahabari kwa ushirikiano mkubwa wa dhati wanaouonesha katika kusimamia masuala ya amani na usalama mkoani Shinyanga.

 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com