Mkurugenzi Mkuu wa Soud Group Company, Hilal Soud
Na Annastazia Paul - Shinyanga
Waumini wa dini ya Kiislamu Mkoani Shinyanga wametakiwa kuishi kwa kufuata misingi ya dini, kwani ni ufunguo wa kutafuta usalama, maisha na inaleta baraka katika maisha yao.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Mei 14 2021, na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Soud Group (Soud Company Group) Hilal Soud wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Shinyanga katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Fitr, ambapo amesema kuwa Waislamu wote wanapaswa kuishi kwa kufuata dini.
“Waislamu wote akina baba, akina mama na watoto, ninawaasa kila mmoja afuate dini, kwani dini ni ufunguo wa maisha yake, dini ni ufunguo wa kutafuta usalama, dini inaleta baraka na ndiyo maana unakuta dini imepewa kipaumbele na huwa haiingiliwi na msimamo wa dini unaleta kheri”,amesema.
Amewaomba watu wenye uwezo wa kusimamia mambo ya dini waendelee kujitoa ili yasonge mbele.
“Waliopewa na Mungu, kwa mkono wa kulia nao watoe ili mambo ya dini yasonge mbele .Kwa waumini nawataka waendelee ili waweze nao kuwa wengi, kadri tunavyowasogezea majengo ya dini basi waumini waweze kuendelea na watatupa uwezo wa kufikiria kuwa kuna usalama zaidi”,amesema Hilal.
Hilal Soud ambaye pia ni Mjumbe wa Taasisi ya Kiibadhi ya Istiqaama Muslim Community of Tanzania inayojihusisha na masuala mbalimbali ikiwemo uratibu wa miradi ya kusaidia uislamu, kutoa elimu ya dini ya kiislamu, kujenga na kusimamia madrasa,misikiti shule na vituo vya kulelea yatima, amesema wanaendelea na ujenzi wa misikiti katika maeneo ya Kenyata na Ushirika Mjini Shinyanga.
Amesema kuwa wana mpango wa kusaidia watu mbalimbali hasa waamini wa dini ya kiislamu kupitia miradi ambayo itakuwa ikifanyika katika misikiti hiyo.
“Kujengwa kwa msikiti katika eneo la Kenyatta tunataka tuunganishe na madarasa ya akina mama, kwa sababu kubwa nyingi, sababu ya kwanza akina mama ni watu ambao wakipata elimu maana yake watoto wamefikiwa, jambo la pili ni watu ambao wanazingatia dini sana na pia Shinyanga tumeona akina mama wengi bado hawajaelewa dini inavyotakiwa, Msikiti huo unajengwa na familia ya Hilal Soud ambayo imeamua kusaidia jambo hilo litakalowanufaisha Waislam hasa katika Mkoa wetu wa Shinyanga”, ameeleza Hilal Soud.
Amesema kuwa msikiti uliopo katika eneo la Ushirika mjini Shinyanga unajengwa kwa michango ya Waislam mbalimbali walioamua kujitoa kwa usimamizi wa taasisi Kongwe ya Istiqaama Muslim Community of Tanzania na kwamba kutakuwa na madarasa pamoja na kituo cha kulelea watoto yatima.
“Huo Msikiti wa Ushirika unajengwa lakini kuna ndugu zangu wengi ambao wanausimamia ambao wapo karibu na sisi na pili Jumuiya itakuwa nayo inachanga katika jengo hilo na pia msikiti huo unajengwa na wasali waumini wa kiislam kwa kiasi kinachowezekana, pia tunatajia kutakuwa na madarasa mchanganyiko na kituo cha kulelea watoto yatima”, ameongeza.