Kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei imetoa wito wa
uwepo wa ushirikiano madhubuti baina ya sekta za umma na sekta binafsi ili
kurejesha imani baina ya sekta hizo mbili kwa mustakabali mzima wa uboreshaji
wa teknolojia.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Makamu Mwandamizi wa
Rais na mwanachama wa bodi ya wakurugenzi ya Huawei, Catherine Chen kwenye Kongamano la Mtakatifu Gallen - mkusanyiko wa
viongozi wa sasa na wa baadaye kutoka kote ulimwenguni ambao hufanyika kila
mwaka.
Kongamano hilo lililenga kusherehekea kumbukumbu ya miaka
50 tangu kuanzishwa kwake. Katika kongamano hilo, jumla ya watu 1,000
walishiriki kwenye mazungumzo ya siku tatu baina ya vizazi tofauti kutoka Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Gallen, kituo cha kimataifa Singapore, Balozi kumi za
Uswizi kote ulimwenguni, na mahali pengine mtandaoni.
Wasemaji wengine kwenye kongamano hilo ni pamoja wakuu
mbalimbali kutoka sekta binafsi ambao ni pamoja na Christophe Franz, Mwenyekiti
wa bodi ya Roche, Ola Källenius, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi huko Daimler,
Satya Nadella, Afisa Mtendaji Mkuu wa Microsoft, na Roshni Nadar Malhotra,
Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la HCL.
Washiriki, ambao pia walijumuisha viongozi wa kisiasa, kama
vile Kansela wa Austria, Sebastian Kurz, na wawakilishi wa mashirika ya
kimataifa, kama Mwenyekiti wa mpango wa kidijitali Uswizi, Doris Leuthard,
walikusanyika kubadilishana maoni yao juu ya mada ya kongamano la mwaka huu,
"Uaminifu ni Muhimu" kitu ambacho Huawei imejitolea sana.
Kwa mujibu wa Chen anaamini inahitajika juhudi za pamoja za
watunga sera, wasimamizi, na sekta binafsi. "Kwa kuwa vifaa vingi
vinajumuisha mawasiliano, uwepo wa ongezeko la huduma kwa njia za mitandao
pamoja na miundombinu muhimu kutegemea upatikanaji wa data kwa wakati halisi,
ni lazima kwa serikali zote ulimwenguni kuhakikisha kuwa kila mtu analindwa kwa
kiwango cha juu kabisa kiusalama. Kitu pekee kinachoweza kuleta imani katika
teknolojia ni uwepo wa sheria moja na jumuishi kwa nchi zote,” alisema.
Kongamano hilo kwa mwaka huu lilianza Mei 5. Washiriki wa
hafla hiyo walikubaliana kwamba uaminifu hujengwa kwa uwazi, na kwamba ni
wakati wa kuchukua hatua madhubuti kushughulikia changamoto hiyo na hatari
ambazo zimeibuka baada ya janga la COVID-19.
Uaminifu wa umma katika taasisi za kisiasa na kiuchumi,
teknolojia zinazoibuka, na vyombo vya habari vimeharibiwa hivi karibuni, haswa
kati ya kizazi cha vijana, na hii imezidishwa na janga la COVID-19.
"Sisi, kwa kizazi chetu, tunaunganishwa na idadi kubwa
ya watu kupitia mitandao ya kijamii, lakini hii haimaanishi ni kundi la watu
ambao tunaweza kuwaamini," alisema Simon Zulliger, mshiriki wa timu ya
wanafunzi 35 kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Gallen ambacho kiliandaa kongamano
la mwaka huu. Timu hiyo ilielezea maoni yao kuwa kutafuta njia za kuhifadhi na
kuimarisha uaminifu ni muhimu kwa kurudisha imani.
Chen anatumaini kwamba kizazi kijacho cha viongozi kitaunda uaminifu na kuunda ulimwengu uliounganishwa kimtandao. "Ninawahimiza waendelee kukuza uhusiano mzuri kati ya jamii, watu, na mazingira yao. Lazima tujenge imani kubwa katika teknolojia, iliyowezeshwa na ya sheria jumuishi, ubunifu na maendeleo. Hapo tu ndipo tunaweza kujitolea kwa matumizi endelevu na ya kuaminika ya teknolojia," alisema.