ATUPWA JELA MIAKA 200 KESI YA UHUJUMU UCHUMI TANZANIA


Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, imemhukumu Semeni Gwewa Mswima ambaye alikuwa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mlowo, kifungo cha miaka 200 Jela au kulipa faini ya Sh.52,000,000 pamoja na kurejesha kiasi cha Sh.30,850,000 alichoiibia Halmashauri Wilaya ya Mbozi.

Kesi hiyo ambayo ni kesi ya Uhujumu Uchumi Na.01/2021 ilifunguliwa na TAKUKURU Mkoa wa Songwe mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya hiyo, Vitalis Changwe ambapo mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na makosa 60 ambapo ndani yake kuna makosa ya kutumia nyaraka za uongo kinyume na kifungu cha 342 na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2019 na makosa ya wizi kwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258(1) na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Mwaka 2019.

Akisomewa Mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Mkoa wa Songwe, Emanuel Ndembeka akisaidiana na Simona Mapunda, alieleza mahakamani hapo kwamba mshtakiwa kwa tarehe tofauti tofauti kati ya tarehe 04/07/2019 hadi tarehe 08/05/2020 kwa kutumia hati za malipo na hundi zilizoghushiwa aliweza kutoa na kuiba fedha jumla ya Sh.30,850,000 toka katika akaunti Na.61210014674 ambazo ni mali ya Halmshauri ya Wilaya ya Mbozi.

Mshtakiwa alikiri makosa yote 60 yaliyokuwa yakimkabili.

Akitoa hukumu hiyo,Hakimu Changwe alimwamuru mshtakiwa kulipa faini ya Sh.800,000 au kwenda jela miaka mitatu kwa kila kosa la kuwasilisha nyaraka za uwongo,ambapo kulikuwa na jumla ya makosa 40.

Hakimu huyo pia alimwamuru mshtakiwa alipe faini ya Sh.1,000,000 au kwenda jela miaka minne kwa kila kosa la wizi kwa mtumishi wa umma ,ambapo kulikuwa na jumla ya makosa 20. Pamoja na kulipa faini hizo,Mahakama ilimwamuru mshtakiwa ajereshe katika halmashauri husika fedha alizoiba kiasi cha Sh. 30,850,000, mshtakiwa alishindwa kulipa fedha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post