Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma
Mheshimiwa George Yambesi amewataka Watumishi wa Kampuni ya Uendelezaji wa
Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KADCO) kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Yambesi amesema haya leo Mkoani
Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa KADCO kuhusu
utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na usimamizi wa Utendaji
Kazi kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS) yaliyoandaliwa
na KADCO na yanatolewa na wawezeshaji
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma.
Alisema, watumishi wa KADCO wanatakiwa
kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma kwa kufanya kilicho
sahihi huku wakizingatia utaalamu, uaminifu na uwajibikaji katika utendaji kazi
wao wa kila siku wakati wa utoaji huduma.
“Naipongeza Menejimenti ya KADCO kwa
kuandaa mafunzo haya kwa Watumishi ambayo
naamini yataboresha utendaji kazi wenu na uzingatiaji wa Sheria wakati wa
ushughulikiaji wa haki na wajibu wenu na wa wengine wakati wa utoaji wa huduma
katika uwanja wetu wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA). Ni muhimu wakati
wote mkafahamu kuwa nyinyi ni Taasisi ya kibiashara, wakati wote mnatakiwa kwa
mbele kiushindani ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ” amesema.
Mheshimiwa Yambesi amesema kuwa hakuna
Haki isiyo na Wajibu, Waajiri wana wajibu wa kuhakikisha watumishi wa umma wanapata
stahili zao zote za kiutumishi ambazo ni haki yao kwa wakati na watumishi wana
wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za
Utumishi wa Umma ambayo ni haki ya Waajiri.
“Hivyo,
ni muhimu kwa watumishi wa umma kupandishwa
vyeo, kuthibitishwa kazini na kulipwa stahili zao mbalimbali kwa wakati na kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Aidha, Watumishi wa
Umma wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu, uadilifu na kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kupata stahili
zao” amesema.
Kamishna Yambesi amesema miongoni mwa
majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma ni
pamoja na kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria,
Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma; Kupokea na kushughulikia rufaa za
mashauri yaliyotolewa maamuzi na Mamlaka za Nidhamu; Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji
kazi wa watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia
matokeo.
Akizungumzia
kuhusu OPRAS Mheshimiwa Yambesi amesema OPRAS ipo kisheria ni vizuri watumishi wa
KADCO na watumishi wa umma wakaielewa vizuri ili kila mtumishi aweze kupimwa
utendaji wake na apate anachostahili kwa
haki bila upendeleo na upandishwaji cheo
kwa mtumishi kutokane na ufanisi wake
katika utendaji wa kazi.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (KADCO) Dkt. Natu Mwamba
amesema mafunzo haya yanafanyika kipindi ambacho KADCO inaandaa Mpango Mkakati
wa Miaka mitano ijayo ni imani kubwa kuwa malengo ya Tasisi yatakayowekwa yatakuwa
ni yenye kutekelezeka na mtiririko wake utakwenda vizuri hadi kwa wafanyakazi ili
waweze kuweka malengo yanayopimika katika utendaji kazi wao.
Awali
akizungumza wakati wa kumkaribisha mheshimiwa Yambesi, Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe amesema anaishukuru Tume ya
Utumishi wa Umma kwa kukubali kuja kutoa mafunzo haya. Mafunzo haya yanafanyika
baada ya Tume kufanya ukaguzi wa masuala ya Rasilimali watu KADCO na kubaini
uwepo wa baadhi ya mapungufu. Menejimenti ya KADCO inatarajia mafunzo haya yatakuwa ni yenye
tija na yataongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Amesema jumla ya watumishi
291 wanatarajia kushiriki katika mafunzo haya ya wiki mbili.
Imeandaliwa na:
KITENGO
CHA MAWASILIANO SERIKALINI
TUME
YA UTUMISHI WA UMMA
KADCO-KILIMANJARO
10
MEI 2021
Social Plugin