Eneo la harusi
**
Kisanga kilizuka katika harusi eneo la Mwatate, Taita Taveta nchini Kenya baada ya jamaa 'Mshereheshaji/MC) aliyekuwa akisimamia sherehe hiyo kushindwa kuzungumza na kulazimika kutupa Kipaza sauti (maikorofoni) alipogundua ni Mpenzi wake wa zamani (Ex wake) aliyekuwa akiolewa.
Penyenye zinasema kuwa kisura alimtoroka jamaa kwa dharau akimwambia kwamba hawezi kuolewa na mtu maskini.
Kulingana na Taifa Leo, jamaa huyo ni mwalimu na wengi walimjua sana kutokana na sauti nzuri na maneno ya kumtoa nyoka pangoni ila siku hizo alibaki amekauka mdomo.
Inasemekana kuwa kisura aliyekuwa akiolewa alikuwa mpenzi wa zamani wa barobaro huyo.
Licha ya jamaa kujibidiisha kupiga vibarua na kumfurahisha mrembo huyo, bado aliachwa kwenye mataa.
Duru zinaarifu kwamba jamaa alipogundua anaongoza harusi ya mpenzi wake wa zamani aliyempenda kwa dhati aliingiwa na huzuni mwingi akashindwa la kusema.
Penyenye zinaarifu kwamba wawili hao hawakukosana walipoachana ila mrembo alijiondoa kwa upole na kuanza uhusiano na jamaa mwingine aliyekuwa na donge nono mfukoni.
“Heri niolewe na rubani. Mwalimu kama wewe unayekisifia Kiswahili chako na sauti nzuri utanipa nini?” jamaa alikumbuka mrembo akimuuliza na hapo akaishiwa nguvu mwilini na kuangusha kipaza sauti.
Aliinama akakiokota lakini akaanza kukohoa, hata maji aliyoletewa hayakumfaa kitu.
Hatimaye lofa aliamua kukabidhi maikorofoni akiashiria kwamba hangeendelea na sherehe, huku kisura akionekana akimtazama na kutabasamu akifurahia mateso ya jamaa.
“Alinikataa aolewe na jamaa yule mwenye sura ya nyani! Jamani! Kumbe pesa ni sabuni ya roho!” jamaa alisikika akisema huku akisaidiwa kuondoka jukwaani kwani alikuwa ameisha nguvu kabisa.
Waliomsikia walimuonea huruma ila hakuna jinsi wangeweza kumsaidia.
“Mbona wanawake wanatesa majamaa hivi jamani?” jamaa mmoja alisema kwa huruma. “Lakini pia ukiachwa achika tu na ukubali,” mrembo mmoja naye alimjibu.
Semasema zinaarifu kwamba jamaa alipopata mpenyo, alitumia mlango wa nyuma kutoweka katika sherehe hiyo.
CHANZO - TUKO NEWS
Social Plugin