Baadhi ya madereva wakifungua shehena ya mazao mbalimbali baada ya amri ya Mkuu wa wilaya ya Singida Mjini Mhandisi Paskas Muragiri kuwataka kufungua ili kuona kilichomo ndani yake baada ya gari moja kudanganya kuwa limebeba pumba kumbe limebeba mchele
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini Paskas Muragili (katikati) akizungumza na madereva wa maroli hayo
Mkuu wa wilaya ya Singida Mjini Mhandisi Paskas Muragiri akisikiliza maelezo kutoka kwa madereva hao
Na Edina Alex, Singida
Mkuu wa wilaya ya Singida Mjini Mhandisi Paskas Muragiri amekamata shehena zenye zaidi ya tani 40 ya mazao mchanganyiko ambayo yanadhaniwa kupitishwa katika mkoa wa Singida bila kutoa ushuru.
Magari hayo yaliyobeba shehena hizo yenye namba za usajiliT 335 AWH,T178CBB,T662DTL,T489DUV na T850AFQ yamekamatwa eneo la Njia panda katika kata ya Mughamo Wilaya ya Singida yalipokuwa yakivuka eneo hilo kutokea Mkoa wa Kagera kwenda Jijini Arusha.
"Tumekamata Magari matano ambapo kila gari lilikuwa na magunia zaidi 250 ya Maharage na mchele ambayo hayakulipiwa ushuru wa mazao", alisema Muragiri.
Alisema mpaka sasa shehena hizo zinashikiliwa hadi pale watuhumiwa watakapo kamilisha malipo ya faini na ushuru kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Halmashauri.
"Ili kukomesha vitendo hivyo tumelazimika kuwatoza faini ya shilingi laki mbili kwa kila gari ,lakini pia watatakiwa kulipa ushuru wa shilingi elfu 3 kwa kila gunia kwa idadi ya magunia yote yapatayo elfu 3,"alieleza Muragiri.
Kwa upande wao wananchi akiwemo diwani mstaafu wa kata ya Unyambwa iliyopo Manispaa ya Singida Hamis Labu wanaozunguka eneo hilo wameishukuru serikali ya Mkoa kwa jitihada hizo za udhibiti wa utoroshwaji wa vyanzo vya mapato kwa lengo la kusaidia ustawi wa maendeleo .
"Tunaishukuru serikali yetu kwa kuwa na watendaji wenye weledi katika kuhakikisha kuwa Halmashauri zetu zinakuwa kiuchumi kwa kukusanya mapato",alisema Labu.
Social Plugin