Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA MIPANGO MIJI HALMASHAURI YA SHINYANGA YAZINDULIWA....DED MAHIBA ATAMANI ISELAMAGAZI UWE MJI WA SERIKALI


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akizungumza wakati akizindua Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba amezindua Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo huku akiwasisitiza wajumbe kutumia taaluma zao vizuri kupanga ardhi na kuwa chachu ya kusuluhisha migogoro ya ardhi.

Uzinduzi huo uliokwenda sanjari na kikao cha kwanza cha Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga umefanyika leo Alhamis Mei 20,2021 katika Ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizindua Kamati hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba amewataka wajumbe wa kamati hiyo wakatekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa.

“Wakati tunafanya uchambuzi wa majina tulizingatia vigezo,tuliona kuna vitu tofauti kwenu ambavyo mnaweza kutusaidia sisi kama Menejimenti kuweza kuivusha salama Halmashauri yetu. Mmeteuliwa kwa kuzingatia taaluma zenu. Ukiangalia asilimia kubwa ni vijana,bado ni nguvu kazi mnaweza kufanya kazi zenu vizuri na taifa linawategemea”,amesema Mahiba.

“Kati ya halmashauri chache kama siyo Halmashauri ya kwanza mkoa wa Shinyanga sisi ni wa kwanza kuzindua kamati hii. Sisi tumefanya haraka baada ya kupata waraka kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa hii kamati kwa sababu sisi ni kati ya watu ambao tuna eneo kubwa sana ambalo tunahitaji kulipanga”,ameeleza Mahiba.

Ameitaja sababu nyingine iliyowafanya wazindue kamati ya mipango miji haraka ni kutokana na kwamba halmashauri hiyo ya Shinyanga ni mpya kwa maana ya mazingira,wamehamishiwa hapo sasa takribani mwaka mmoja hivyo tunahitaji kupanga mji wetu na maeneo mengine ambayo yamekuwa ‘Planning areas’ na kwamba kwenye upande wa ardhi bado wana maeneo mengi yanayohitaji kupangwa hali iliyowafanya waone umuhimu wa kukimbia kuandaa kamati ili ianze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

“Kamati hii ndiyo dira ya halmashauri, mkipanga vibaya maana yake na matumizi yatakuwa mabaya, mkipanga vizuri matumizi yatakuwa mazuri. Mkafanye kazi kama wataalamu, mnapopanga mjiridhishe,mkague, mridhike na kile mnaenda kukitolea maamuzi. Naomba mkawe chachu ya kusuluhisha migogoro ya ardhi”,amesema Mahiba.

“Kamati hii ni kamati ya wataalamu,kuna taaluma mbalimbali hapa na suala la ardhi ni suala mtambuka. Tuna majukumu ya kupanga ardhi yetu iwe ardhi endelevu. Sasa kwa hilo jukumu mkalifanye vizuri. Natamani makao makuu ya halmashauri hapa Iselamagazi siku moja tuwe na mji wa Serikali, tuwe na mji ambao umepangwa vizuri”,ameongeza Mahiba.

Aidha ameitaka kamati hiyo ikawe chachu ya kuvutia wawekezaji kupitia ardhi iliyopo akisisitiza wapange ardhi vizuri na kuweka utaratibu vizuri.

“Wananchi wengi bado wanahitaji kuelewa thamani ya ardhi waliyonayo na wakati mwingine wanaingia kwenye migogoro kwa sababu ya kutokuwa na ufahamu hivyo kamati ina jukumu la kuwaelimisha wananchi. Kamati hii haipangi tu bali inawashirikisha wadau hivyo mipango yenu ikawe shirikishi ili kuwa na mipango mizuri na mipango shirikishi ili kuitengeneza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ikawa na mipango mizuri ya ardhi na yenye tija kwa wananchi na ni endelevu kwa ustawi wa jamii.

“Kwa yale maeneo ambayo wananchi wameshajenga urasimishaji uendelee lakini kwa yale maeneo ambayo hayajapangwa tuyapange vizuri, sisi ndiyo kamati ambayo tunaweza kusema hiki ni sawa,hiki siyo sahihi turekebishe. Lakini pia mna mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi,unaweza kukuta mtu amepewa ardhi yake kwa ajili ya kujenga kiwanda halafu kesho anakuja anasema anataka kufanya kilimo. Tutumie taaluma zetu vizuri katika hilo eneo lakini pia tuangalie mahitaji yetu ni yapi”,ameeleza.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa kuwapongeza Viongozi wa kamati hiyo akiwemo Bi. Emelda Kilima (Mwenyekiti) ambaye ni Afisa Mipango wa halmashauri hiyo, Julius Mashauri Maira (Katibu) ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri hiyo na Mhandisi Hassan Koko kutoka TANESCO (Makamu Mwenyekiti).

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bi. Emelda Kilima amesema wapo tayari kutekeleza majukumu waliyopewa wakishirikiana watalaamu mbalimbali wa halmashauri hiyo.

Awali akizungumza Katibu wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Julius Mashauri Maira ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Halmashauri hiyo amesema kamati hiyo inaundwa na wajumbe wasiopungua nane wala kuzidi 15 kutoka sekta ya ardhi,mamlaka za upangaji,taasisi za serikali zinazotoa huduma.

Ameyataja baadhi ya majukumu ya kamati hiyo kuwa ni kukagua na kupitisha mipango ya jumla na ya kina inayokidhi vigezo kwa ajili ya kuidhinishwa na ofisi ya ardhi mkoa na kutoa mapendekezo ya mipango ambayo itakuwa haikidhi vigezo vya kuidhinishwa na kuratibu usimamizi na utekelezaji wa mipango ya jumla na ya kina iliyoidhinishwa.

Majukumu mengine ni kutoa mapendekezo ya maeneo yaliyoiva kwa ajili ya urasimishaji,kushauri juu ya maeneo muhimu katika mamlaka za upangaji,kukagua na kupitisha maombi ya mabadiliko ya matumizi ya ardhi na kukagua maeneo yanayotiliwa mashaka ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati akizindua Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma yao. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,  Julius Mashauri Maira akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bi. Emelda Kilima. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati akizindua Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati akizindua Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo
Katibu wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,  Julius Mashauri Maira akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba (kulia) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,  Julius Mashauri Maira akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bi. Emelda Kilima.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bi. Emelda Kilima akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi Hassan Koko, kushoto ni Katibu wa Kamati hiyo, Julius Mashauri Maira
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Bi. Emelda Kilima akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhandisi Hassan Koko, kushoto ni Katibu wa Kamati hiyo, Julius Mashauri Maira
Katibu wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,  Julius Mashauri Maira akizungumza leo Alhamis Mei 20,2021 wakati wakikao cha kwanza cha Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo.
Wajumbe wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga waliohudhuria uzinduzi wa kamati hiyo wakiwa ukumbini
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba (wa pili kulia waliokaa) akipiga picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga waliohudhuria uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba (wa pili kulia waliokaa) akipiga picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Mipango Miji halmashauri ya wilaya ya Shinyanga waliohudhuria uzinduzi huo.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com