Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHINDANO LA MISS KAHAMA 2021 KUFANYIKA JUMAMOSI JUNI 5...WAREMBO 12 KUCHUANA


Mkurugenzi wa Kampuni ya Br.Black Social Partners , Peter Frank Alex akizungumzia kuhusu maandalizi ya Shindano la Miss Kahama 2021. Kushoto ni Katibu wa Taasisi ya Urembo ya Miss Tanzania (Miss Tanzania Organization) na The Look Company Limited, Benard Mwata.

 Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Shindano la Urembo kutafuta mlimbwende wa Kahama ‘Miss Kahama 2021’ yanatarajia kufanyika June 5,2021 katika ukumbi wa African Lounge Mjini Kahama yakishirikisha warembo 12 huku Msanii Mr. Blue akinogesha mashindano hayo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Mei 28,2021, Mkurugenzi wa Kampuni ya Br.Black Social Partners ambao ni waandaaji wa Shindano la Urembo la Miss Kahama, Peter Frank Alex amesema maandalizi ya shindano hilo yamekamilika.

Amesema shindano la Miss Kahama litafanyika Jumamosi June 5, 2021 African Lounge. Washiriki wapo 12 ambao ni mabinti warembo kutoka Kahama ambao sasa wapo kambini wanaendelea na mazoezi.

“Maandalizi ya shindano la Miss Kahama ni makubwa hivyo wananchi wategemee mambo makubwa siku hiyo kuanzia saa moja usiku. Tiketi zinaendelea kutolewa maeneo mbalimbali ikiwemo Huheso FM kwa Zakazi, BSL College, African Lounge na tunasambaza mtaa kwa mtaa na siku ya shindano tiketi zitapatikana getini”,amesema.

“Sisi kama waandaaji wa Miss Kahama tumekaa na Waandaaji Wakuu wa Miss Tanzania na tumepewa taratibu na vigezo mbalimbali hivyo. zile sintofahamu ambazo zilikuwa zinaendelea mtandaoni tumeshazirekebisha hivyo Shindano la Miss Kahama lipo kama kawaida tarehe 6 Mwezi wa Sita”,ameongeza Alex.

Ameeleza kuwa wameandaa zawadi na fursa mbalimbali kwa washiriki wa shindano la Miss Kahama ambazo zitawasaidia katika maisha yao huku akiwaomba wakazi wa Kahama na maeneo ya jirani kujitokeza kushuhudia shindano hilo.

Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Urembo ya Miss Tanzania (Miss Tanzania Organization) na The Look Company Limited, Benard Mwata amesema mwaandaaji wa shindano la Miss Kahama amekamilisha taratibu zote hivyo ana Baraka zote za kuendesha shindano hilo June 5, 2021.

“Waandaji wa shindano la Miss Kahama wameshakamilisha taratibu zote zilizokuwa zinatakiwa hivyo Mkurugenzi wa Br.Black Social Partners ,Peter Frank Alex ni mtu rasmi kwa ajili ya kuandaa shindano hilo Kahama kwa ajili ya kunyanyua vipaji vya watoto wa kike pamoja na vipaji vingine ndani ya Kahama”,amesema Mwata.

“Mwenzetu ameweza kuandaa maandalizi ya Miss Kahama. Kwa hiyo mimi kama Mwakilishi wa Miss Tanzania Organisation napenda kuwataarifu kuwa tumemruhusu Mkurugenzi wa Br.Black Social Partners ,Peter Frank Alex kufanya shindano la Miss Kahama kama chini ya Miss wilaya na utaratibu mwingine utafuata wa kuandaa Miss Mkoa na Kanda kama alivyoelekezwa”,amesema.

Amesema Taasisi ya Miss Tanzania inamchukulia Mkurugenzi wa Br.Black Social Partners ,Peter Frank Alex kama mdau anayeandaa kwa watoto kwa ajili ya kuonesha vipaji vyao katika jamii na kutumia kutangaza utalii na uwekezaji.
Katibu wa Taasisi ya Urembo ya Miss Tanzania (Miss Tanzania Organization) na The Look Company Limited, Benard Mwata akizungumzia shindano la Miss Kahama 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Br.Black Social Partners , Peter Frank Alex ambaye ni Mwandaaji wa Shindano la Miss Kahama 2021.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Br.Black Social Partners , Peter Frank Alex akizungumzia kuhusu maandalizi ya Shindano la Miss Kahama 2021.Kushoto ni Katibu wa Taasisi ya Urembo ya Miss Tanzania (Miss Tanzania Organization) na The Look Company Limited, Benard Mwata.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com