Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MREMBO AFUNGA VIRAGO NA KUMKIMBIA MME WAKE AKIDAI NI MLAFI SANA


Mrembo kutoka mtaani Githunguri, kaunti ya Kiambu nchini Kenya ameamua kufunga virago na kumkimbia mumewe akidai hangevumilia kamwe tabia yake ya ulafi.

 Penyenye zinasema kwamba barobaro alianza tabia hiyo miezi kadhaa iliyopita na haijulikani ni wapi haswa alikotoa tabia hiyo kwa mujibu wa Taifa Leo.

“Jamani, sijui mume wangu amekuwa jini au nini! Nikipakua chakula anakula chote hivi kwamba mimi na wanangu nyakati nyingi tunakosa chakula na kulala njaa," mama alilia. 

Mama huyo alidokeza kwamba hata baada yake kulalamika mara kwa mara mumewe alikuwa akijitia hamnazo na kuendelea kufagia tu chakula chote jikoni.

 “Anakula hadi anavua shati, anakula ovyo na kulala kwenye sofa,” mrembo alieleza kwa masikitiko makubwa.

 Siku ya kisanga inasemekana mama aliandaa chapati kwa kitoweo cha kuku na kwa kuwa alikuwa hodari sana kwa mapishi watoto walikuwa na furaha isiyo na kifani.

Inasemekana kabla ya mama kupakua mlo, jamaa aliingia kwa kishindo.

 “Hujapakua chakula? Wagonja nini wewe jamani?” baba wa nyumba aliuliza kwa hasira. Pindi tu mama alipoweka chapati kwenye sinia, jamaa aliwaashiria watu wote kuketi kando na kumgonja ashibe.

 Inasemekana bila hata kujali watoto, alianza kula chapati kwa kasi huku akizirarua mara mbili tu. Lofa alirarua chapati zote familia yake ikisalia kumtazama. Wanawe walilia wakijishika matumbo, shetani mtu asione hata aibu wala huruma.

Tabia ya jamaa ilimfika kwenye koo mama naye mara moja akaingia chumbani akakusanya virago akawachukua wanawe na kushika njia.

 “Twendeni wanagu hapa tutakufa njaa,” aliwaambia wanawe. “ Mnaenda wapi nyinyi?” lofa aliuliza huku chapati ya mwisho ikiwa kinywani. “Hukunitoa pangoni. Nina kwetu na ndiko ninakoenda,” mama alimjibu jamaa kwa ujeuri kisha akaondoka.

 “Watarudi tu. Lakini hii tabia yangu itakuja kuniua maskini mie. Nitaikomeshaje jamani? Najipata nala tu bila breki!” jamaa alimweleza rafiki yake siku iliyofuata. Hata hivyo haijulikani iwapo mke na mume walisuluhisha tofauti zao na kurejea nyumbani na watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com