Mtangazaji maarufu wa televisheni ya NBS nchini Uganda Sheilah Nakabuye alifariki dunia saa chache baada ya kujifungua mtoto wa kike.
Sekta ya utangazaji nchini Uganda inaomboleza kufuatia kifo cha mmoja wa waandishi wa Habari Sheila Nakabuye kilichotokea Jumatatu, Mei 17, 2021.
Kifo cha Sheila ambaye alikuwa na umri wa miaka 32, kimejiri siku moja baada ya kujifungua mtoto wa kike, aliripotiwa kupoteza fahamu pindi alipofanyiwa upasuaji.
Kulingana na ripoti ya daktari katika kliniki ya Cedus, marehemu alipatikana na matatizo ya uvimbe kwenye mishipa ya ubongo.
Mamake alisema bintiye alipoteza fahamu na alipokimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Mbarara, alikata roho saa chache baada kuhudumiwa na madaktari.
" Kama hali hiyo ingeshughulikiwa kwa wakati ufaao ama kwa dharura, nadhani binti yangu hangepoteza maisha yake, ripoti ya daktari inasema aliangamizwa na uvimbe kwenye mishipa ya ubongo," Mamaake Sheila alisema.
Mtangazaji mwenzake Ambrose Muhumuza alisema kabla ya kulemewa, Sheila alijaribu kula vitafunio lakini alitapika na alionekeana mdhaifu sana.
Kwa mujibu wa taarifa za Daily Monitor, babaake marehemu Mzee Matovu alizirai na kukimbizwa hospitalini baada ya kupokea habari za kifo cha bintiye.
Viongozi wa tabaka mbali mbali, marafiki na watangazaji wenzake wameomboleza kifo chake kupitia mitandao ya kijamii.
Sheilah tayari amezikwa kulingana na desturi ya dini ya kiislamu eneo la Kabasanda wilaya ya Butambala.
Social Plugin