Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWAKINYO KUMPA ASANTE RAIS SAMIA KWA KUMCHAPA MAYALA


Mabondia wa kigeni na makocha mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja tayari kwa kupambana na wapinzani wao wa Tanzania katika pambano la Rumble in Dar 2 lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports.

***

Bondia Hassan Mwakinyo ameahidi kumpa kipigo kikali mpinzani wake Antonio Mayala kutoka Angola ikiwa asante kwa Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Mwakinyo ambaye atawania mkanda wa Afrika (ABU) wa uzito wa Super welter atapanda ulingoni kesho kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki katika pambano lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports.

Alisema kuwa amejiandaa vyema na kwa vile atakuwa anapigana kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wa Rais Samia, hatofanya makosa zaidi ya kushinda katika raundi za mwanzoni tu katika pambano hilo lililodhaminiwa na KCB Bank, Plus TV, Multichoice Tanzania, Tanzania Tourism Board, Onomo Hotel, Precision Air, Prestine Logistics, Urban Soul na washirika wa kimataifa Global Boxing Stars na Epic Sports Entertainment.

“Nitakuwa napigana kwa mara ya kwanza chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Sitamwangusha Rais na watanzania kwa ujumla, nawaomba mashabiki kufika kwa wingi ili kunipa sapoti,” alisema Mwakinyo.

Wakati Mwakinyo anasema haya, mpinzani wake Mayala amesema kuwa pamoja na kupata taarifa za muda mfupi, amejiandaa vyema ili kuonyesha kuwa yeye ni bondia wa ngumi za kulipwa.

“Nimekuja kwa ajili ya kushinda na si kupoteza, nilikuwa nafanya mazoezi kwa sababu ngumi ni kazi yangu na siwezi kuruhusu Mwakinyo kushinda na kuchukua mkanda wa Afrika,” alisema Mayala.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema kuwa mbali ya pambano hilo, pia bondia Daniel Matefu atazichapa na bondoa kutoka Bulgaria Pencho Tsvetkov huku bondia wa kike Leila Yazidu atazichapa na bondia wa Bulgarian Joana Nwamerue.

Pia bondia Hamisi Palasungulu atazichapa na bondia wa Congo Brazzaville Ardi Ndembo huku Imani Daudi Kawaya akionyeshana kazi na bondia kutoka Afrika Kusini Chris Thompson.

Pambano lingine la ABU litakuwa kati ya bondia Shabani Jongo chini ya Mnigeria Olanrewaju Durodora ambao watawania uzito wa juu na nyota mwingine Ibrahim Class atazipiga na bondia wa Afrika Kusini, Sibusiso Zingange.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com