********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Waziri wa Uwekezaji Mhe.Geofrey Mwambe ametoa siku 14 kwa wawekezaji nchini ambao shughuli zao za uwekezaji zimesimama au zimekwazwa kutokana na maamuzi ya taasisi za Serikali kuandika barua na kuzipeleka wizarani ili kuweza kushughulikiwa.
Ameyasema hayo leo mara baada ya kutembelea Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuzungumza na waandiahi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Mhe.Mwambe amesema "Kuna wawekezaji ambao wamekuja na kuanguka hawakufanikiwa kuweza kupata idhini ya kuwekeza hivyo hawa wawekezaji wote waje waandike barua kwetu tutakaa ndani ya wizara tutajadiliana na kuona ni namna gani ya kuwasaidia kutoka pale walipokwama kwenda mbele".
Aidha, Mwambe amesema kuwa sekta binafsi inamadhaifu mengi hivyo amewataka wawe wamoja kwa kushirikiana ili kukuza uwekezaji hapa nchini.
"Sekta binafsi acheni kutoa Rushwa hivyo mjikite zaidi katika ulipaji kodi ili kuweza kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini". Amesema Mhe.mwambe.
Pamoja na hayo Mhe.Mwambe ameziomba taasisi za Serikali kushirikiana kuyajenga makampuni ya kitanzania yaliyosajiliwa na kufanya kazi hapa nchini ili kuwasababishia wapate faida na serikali ipate fedha nyingi.
Hata hivyo Mhe. Mwambe amewaonya baadhi ya wafanyabiashara kuwatumia maafisa wa serikali kuwakandamiza wawekazaji wengine ambao wanakuja Tanzania kuwekeza hivyo wakizidi kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.