Queen Cuthbert Sendinga
Na Damian Masyenene - Shinyanga
Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Queen Sendiga ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa mkoa wa Iringa.
Queen Sendiga ambaye alikuwa mgombea wa urais mwanamke kivutio kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ameteuliwa leo akichukua nafasi ya Ali SalimHapi ambaye amehamishiwa mkoa wa Tabora.
Uteuzi huo unakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuahidi kuwa siku za usoni atateua viongozi mbalimbali katika nafasi za uongozi bila kujali itikadi zao za kisiasa bali ataangalia uwezo wao wa kuliletea taifa maendeleo na sifa zao safi.
Rais Samia alitoa kauli hiyo Mei 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam ambapo alieleza kuwa lengo ni kuwa na umoja wa kitaifa.
"Huko mbele wakati nikiendelea kusuka serikali sitaangalia itikadi ya mtu kisiasa. mtu yeyote nitakayeona ana uwezo wa kusaidia taifa letu na kuleta tija katika eneo fulani, nitamteua afanye kazi bila kujali anatoka chama gani. ilimradi tu awe hana dosari ya kiusalama, wala dosari ya kimaadili," alinukuliwa Rais Samia Mei 7, 2020.
Uteuzi wa Queen Sendinga unaleta sura sawa na ule wa Anna Mgwira ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2017 akichukua nafasi ya Said Meck Sadiki, ambapo Anna alikuwa mgombea urais wa Tanzania mwaka 2015 kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Mwaka 2015 Queen aliwania ubunge katika jimbo la Kawe lakini hakufanikiwa kushinda ubunge ambapo jimbo la Kawe lilichukuliwa na Halima Mdee ambaye aliwania ubunge kwa tiketi ya chama cha Chadema.
Queen Sendiga akikabidhiwa fomu ya kugombea urais wa Tanzania mwaka 2020
Social Plugin