Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya (Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja Jijini Nairobi leo tarehe 05, Mei, 2021. PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameliambia Bunge la Kenya kuwa ziara yake nchini Kenya imelenga kukazia maeneo ambayo yalilegalega katika uhusiano wa nchi hizo mbili.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 5, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Kenya mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya.
Mhe. Samia ameuambia mkutano maalumu wa pamoja wa bunge la seneti na bunge la kitaifa nchini Kenya ustawi wa mataifa hayo mawili unaathiri ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa pamoja.
"Kila mara panapotokea kutoelewana kati yetu tunadhoofisha uhusiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bila kukusudia pia tunaathiri utangamano wa Afrika Mashariki, hivyo hatuna budi kuendelea kuelewana",amesema
Rais Samia amesema kuwa kuna kipindi jumuiya hiyo ilijaribiwa kufuatia, maneno na vitendo ambavyo vilipima uimara wa dhamira za nchi wananchama wa jumuiya hiyo kuendelea na safari ya utangamano.
“Ni bahati mbaya kuwa watu hawa wapo katika pande zote mbili, Kenya na Tanzania hutokea pia wachache wao wakawa ni watumishi wa Serikali zetu na hata wanasiasa wa pande mbili za nchi zetu. Bahati nzuri ni kuwa si wengi ndio maana uhusiano wa nchi zetu mbili unatimiza miaka 56 sasa,” amesema Samia.
"Niwahakikishie, mimi na wenzangu nchini Tanzania tutahakikisha kuwa uhusiano wetu unang'ara na kwa kufanya hivyo tung'arishe uhusiano wa Afrika Mashariki. Tanzania itaendelea kuwa jirani na mbia mwaminifu wa Kenya na mwanachama muadilifu wa Afrika Mashariki," amesisitiza Rais Samia.
“Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani Kenya na Tanzania ni wapinzani, mbaya zaidi ni kule kuamini kwao kwamba hilo linawezekana tu mmoja wetu kumwangusha mwenzake, hawa ni watu wenye mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu.
“Ushirikiano wetu si wa hiari bali wa lazima kutokana na kanuni ya uasili wa undugu ambao Mwenyezi Mungu ameuumba, ushirika na ujirani yote yanatufanya tuwe pamoja hili la maumbile hatuna uwezo wa kulibadilisha kilichobaki ama tupendane au tuchukiane hatuwezi kukwepa kutokana na mafundo haya matatu yaliyowekwa pamoja, tunategemeana kwa kila hali iwe kheri au shari”,amesema.
“Panapotokea ukame Tanzania njaa inabisha hodi Kenya, uzalishaji wa viwanda ukisimama Kenya bidhaa zinakosekana Tanzania hivyo hatuna budi kupatana na kuishi kwa neema na furaha,” amesema Samia.