RAIS SAMIA : TUNATARAJIA KUAJIRI WATUMISHI 40,000...MISHAHARA TUTAPANDISHA MWAKANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wafanyakazi mbalimbali katika Kilele cha Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kitaifa ambazo zimefanyika Jijini Mwanza leo tarehe 01 Mei, 2021 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. Picha na Ikulu

**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema jumla ya wafanyakazi zaidi ya 85,000 elfu hadi 91,000 watapanda vyeo mwaka ujao na kuajiri watumishi 40,000 katika Idara ya Elimu na Afya huku akieleza kuwa licha ya matamanio yake ya kuongeza mishahara, Serikali haiwezi kufanya hivyo kwa sasa kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Rais Samia ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa leo Mei 1, 2021 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

"Ndugu zangu mimi ni mama, mama ni mlezi..Dai hili ni la msingi na la kweli. Mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, Mimi binafsi natamani kuongeza mishahara mwaka huu ila kwa sababu mbalimbali nimeshindwa, uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka 6.9% hadi 4.7% kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Imekuwa vigumu kwangu kuongeza mishahara lakini tutaboresha maslahi ya wafanyakazi. Nawaahidi mwakani siku kama ya leo nitapandisha mishahara", amesema Rais Samia.

Hata hivyo katika kuwapunguzia machungu wafanyakazi Rais Samia amesema Serikali imepunguza kodi na tozo mbalimbali katika mishahara ya wafanyakazi.

“Tumeamua kupungzua 1%  ya PAYE kwahiyo sasa Mimi pamoja na nyinyi wafanyakazi wenzangu tutakatwa 8% badala ya ile 9% ya awali.

Kuhusu makato ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, tumeamua kubakia na 15% unayokatwa kwenye mshahara wako na Serikali imeamua kufuta 6% tulizokuwa tukitoza zaidi lakini waliokopa waendelee kulipa, Bodi ya Mikopo naipongeza ila hii 6% waiondoe”,amesema Rais Samia

 Rais Samia pia ameagiza kuundwa mara moja kwa bodi ya mishahara itakayomwezesha kufahamu kiwango cha kuongeza katika mishahara ya watumishi wa umma na sekta binafsi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post