Mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina la Robert Masumbuko (47) mkazi wa Kibirizi Kigoma aliyefariki kwa kunywa sumu wakati akijaribu kuwaaminisha wateja wake kuhusu huduma yake ya kinga ya sumu amezikwa na serikali ya kijiji baada ya mwili wake kuharibika vibaya.
Tukio hilo limetokea katika kijiji cha Isawima kata ya Igagala wilaya ya Kaliua mkoani Tabora tarehe Mei 22, 2021 alipofika ili kutafuta wateja wa dawa zake mbalimbali ikiwemo kinga ya sumu.
Kamanda wa polisi wa Tabora kamishana msaidizi wa jeshi la polisi Safia Jongo marehemu alifariki dunia baada ya kunywa sumu akiwaaminisha wateja wake kuwa akikuchanja dawa kooni hata ukinywa sumu ya aina gani sumu hiyo haiwezi kukufanya kitu wala kufa.
Kabla ya umauti wake mganga Masumbuko alijichanja kwenye koo lake na kisha kunywa sumu akitamba kwamba haitamdhuru.
"Ili kuwahakikishia kuwa dawa yake inafanya kazi aliamua kunywa sumu akamchanja mwananchi mmoja kumpa kinga dhidi ya sumu,huyo mwananchi alipopewa chanjo hiyo akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake hali ilibadilika akapelekwa zahanati kwa ajili ya matibabu, wakati polisi wakifanya utaratibu wa kwenda kumkamata mganga huyo wa jadi kwenye Nyumba ya kulala wageni alipofikia ndipo wakamkuta naye hali yake ni mbaya wakamchukua kumkimbiza hospitali lakini kwa bahati mbaya akafariki dunia",ameeleza Kamanda Jongo.