TBS NA KEBS KUSHIRIKIANA KUONDOA VIKWANZO VYA KIBIASHARA

MASHIRIKA ya viwango ya Kenya na Tanzania yamejipanga kuhakikisha yanashirikiana ili kuhakikisha hakuna vikwazo vya kibiashara vinavyohusiana na viwango vinavyoweza kutokeaa baina ya nchi hizo biashara.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Yusuf Ngenya, wakati wa ziara katika kituo cha pamoja cha mpaka wa Namanga ambayo ilihusisha Mawaziri na Viongozi mbalimbali kutoka nchi za Tanzania na Kenya.

Ziara hii kwa viongozi imefanyika baada ya kukamilika kwa Mkutano wa tano baina ya Tanzania na Kenya kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya biashara ikiwemo vikwazo vya biashara.

Mkutano huo uliofanyika kuanzia Mei 26 hadi 29, mwaka huu jijini Arusha Alisema wao kama TBS na wenzao wa Kenya (KEBS) walizungumzia masuala yanayohusiana na viwango na waliyaweka vizuri.

Alisema kwenye mkutano huo alizungumza mambo mengi ya Afrika Mashariki yanayohusiana na viwango ambayo yameweka vizuri, kwani kuna viwango ambavyo wamepitisha kwa pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeishaweka wazi kwamba inataka kufungua nchi kibiashara na kutoa wito wa kushirikiana baina ya Kenya na Tanzania.

"Kwa upande wa pande hizi mbili (Tanzania na Kenya) kulikuwa na vikwazo ambavyo vinahusiana na viwango na hivyo tumeishazungumza na wenzetu wa Kenya na tumeishayaweka vizuri na Serikali ya Awamu ya Sita imeweka wazi muelekeo wake wa kibiashara," alisema Dkt. Ngenya na kuongeza;

"Na sisi tutashirikiana na KBS kuhakikisha hakuna vikwazo vya kibiashara vinavyoweza vinavyoweza kutokana na TBS au KEBS."

Kwa upande wake Bw. Gervas Kaisi, Meneja wa Uthibiti Ubora TBS alisema katika kutatua changamoto za kibiashara baina ya Kenya na Tanzania, wameangalia suala zima la ubora wa bidhaa zinazotoka Kenya kuja Tanzania na zile zinazotoka Tanzania kwenda Kenya.

Alisema hizo changamoto zinatatulika, hivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kutokuwa na wasiwasi.

Alitoa mfano kwamba kulikuwa na changamoto ya mahindi yanayotoka Tanzania kwenda Kenya yaliyokuwa yanazuiliwa mpakani.

"Lakini sasa tumeona kuna umuhimu wa kuwa na vifaa katika hayo maeneo ambavyo vitatupa vipimo vya haraka haraka ili kutuonesha kwamba kuna sumukuvu au hakuna sumukuvu," alisema.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post