Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema nchi yake iko tayari kuwapokea wawekezaji kutoka Kenya nchini mwake huku akiwataka wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kushirikiana na si kushindana ili kuhakikisha uchumi wa mataifa hayo mawili unakua huku akitumia lugha ya utani, “Tanzania kuna Suluhu na Kenya kuna Uhuru.”
Samia ambaye amewahutubia wafanyabiashara kutoka Kenya na Tanzania amesema hakuna nchi inayoweza kunawiri pekee yake bila ushirikiano.
Rais Samia amewatia shime washiriki katika mkutano huo kwa kusema kwamba wawekezaji hawafai kushindwa kuwekeza katika mataifa hayo mawili aliposema;
"Mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna Uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna Suluhu ya kuondosha vikwazo vya biashara kwa hiyo sasa mshindwe nyinyi,” amesema huku akitabasamu na kuwafanya washiriki wa kongamano hilo kucheka.
“Tanzania ipo tayari kuwapokea wafanyabiashara kutokana Tanzania, milango yetu ipo wazi na mikono yetu iko tayari kuwakumbatia. Serikali yangu ipo tayari kuwa daraja katika kuhakikisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi unafanikiwa”,ameongeza.
Rais Samia amesema serikali yake imechukua hatua ya kuleta mageuzi ili kufanya mazingira ya kufanya biashara kuwavutia wawekezaji kutoka Kenya kwa lengo la kutumia fursa zilizopo.
Amesema Tanzania ina ardhi, vivutio vya utalii na raslimali ambazo zinaweza kutumiwa kuboresha hali ya kiuchumi wa mataifa yote mawili.
Social Plugin