Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ametoa uhuru wa kibiashara kwa wawekezaji wa Tanzania kuwekeza nchini Kenya bila kuwa na visa za biashara wala kibali cha kazi na kuwasihi wahakikishe wanazingatia sheria na kanuni zinazofuatwa na wawekezaji wa Kenya.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 5, 2021, nchini Kenya wakati wa ufunguzi wa kongamano la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania ambalo wamelifungua kwa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na kuongeza kuwa watahakikisha wanarahisisha njia zote za ufanyaji biashara.
"Tungependa kuona wawekezaji wengi wa Tanzania waje wafanye kazi zao hapa Kenya, wawekezaji wa Tanzania mjue kwamba mko na uhuru wa kuleta na kufanya biashara zenu hapa bila kuombwa 'business visa' na work permits' ila mfuate sheria na kanuni zilizowekwa na zile ambazo wenzenu wa Kenya pia lazima wazifuate", amesema Rais Kenyatta
Awali pia Rais Kenyatta alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na siyo kushindana, "Tuko na nafasi na nia ya kuhakikisha kwamba tukifanya pamoja tunaweza kuinua uchumi wa Tanzania na Kenya, naamini Mh Rais Samia Suluhu, kwa dhati ya kwamba tukiingia kwa njia ya kushirikiana ushindi utakuwa wa wananchi wa nchi zetu".
Social Plugin