Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ACHARANGWA MAPANGA NA KUIBIWA PESA BAADA YA KUUZA NG'OMBE, WANANCHI WACHOMA MOTO NYUMBA ZA WATUHUMIWA

 

Na Dinna Maningo,Tarime 

Mwita Samson maarufu kwa jina la Mswahili mkazi wa kitongoji cha Kihero kijiji cha Kemakorere kata ya Nyarero wilaya ya Tarime mkoa wa Mara amejeruhiwa kwa kukatwa katwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na vijana watatu na kisha kuchukua fedha zake na kuondoka nazo.

 

Mwenyekiti wa kijiji cha Kemakorere Marwa Chacha Nyabikone amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea muda wa saa nne usiku wa kuamkia leo na kwamba watu wawili waliohusika na tukio hilo walitambuliwa kwa sura na majina na wote walikimbia.

Nyabikone alisema kuwa polisi walifika eneo la tukio nakumchukua Samson na kumpandisha kwenye gari la polisi kumuwahisha hospitali ya wilaya ili kupata huduma zaidi na anaendelea na matibabu.

"Huku kijijini hatuna zahanati,majeruhi alikuwa bado ana ufahamu aliwatambua vijana wawili ambao majina yao tunayahifadhi kwa uchunguzi zaidi ila mmoja ndiyo hakumtambua kwa sura,walimjeruhi kwa kumkata kwa mapanga kiunoni,tumboni,mkononi,kifuani na begani.

Aliongeza "Ilibidi apatiwe huduma ya kwanza kwenye duka moja la dawa wakamshona na kuwekewa bandeji wakati anaendelea kushonwa polisi walifika wakasema ili kumuokoa akapatiwe matibabu hospitali wakamchukua na kuondoka nae na ndugu zake kwa matibabu zaidi,nawashukuru polisi kwa kufika tunaomba wahusika wakamatwe na wawajibishwe kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho.

"Wananchi walikusanyika pamoja na kufatilia nyayo za miguu hadi nyumbani kwa watuhumiwa ambao wengine walitambuliwa na Samsoni aliyejeruhiwa na wakabomoa nyumba na kuteketeza kwa moto, mimi mtu mmoja sikuweza kuwazuia na nikaogopa hata kwenda kwenye tukio ningefanyiwa kitu kibaya maana walijawa na hasira nilichokifanya nimetoa taarifa polisi",ameongeza.

Mmoja kati ya wananchi wa kijiji hicho ambaye hakutaka jina lake litwaje alisema kitendo cha kuchoma mali siyo cha haki kwani watoto na mke hawana makosa na kitendo hicho kitawakwamisha wanafunzi kutokwenda shule baada ya nguo zao za shule kuteketea kwa moto. 

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kihero Paul Emanuel alisema kuwa alipata taarifa muda wa saa nne usiku ya kuvamiwa mwananchi wake nakwamba chanzo cha kuvamiwa ni baada ya yeye kwenda kuuza ng'ombe wake kwenye soko la ng'ombe jana ijumaa, Mei, 21,2021na ilipofika usiku akavamiwa,bado hakijafahamika kiasi halisi cha fedha zilizoibiwa na wanaendelea na ufuatiliaji.

Kutokana na tukio hilo wanakijiji wanaokadiliwa kuwa zaidi ya 200 majira ya saa kumi na moja leo jumamos wakiwa wanapiga yowe waliandamana hadi kwenye nyumba za watuhumiwa wanaodai hukusika na tukio hilo na kisha kubomoa nyumba zao na kuziteketeza kwa moto pamoja na mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hizo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime/Rorya William Mkonda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo tayari mtuhumiwa mmoja anashikiliwa na polisi na wengine wanaendelea kusakwa. 

Mkonda alisema kuwa tayari ametuma askari kwenda eneo la tukio huku akiwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi nakwamba waliohusika kufanya uhalibifu wa mali watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com