RAIA WA BURUNDI MBARONI KAHAMA, MTUMIAJI WA MIRUNGI AKAMATWA BANGI IKINASWA KWA MAMA BONGE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia Watuhumiwa wawili raia wa nchini Burundi Ndaikenguche Jelala (17), Mkulima na Sezero Dami (16) kwa kosa la kuingia nchini bila kibali pamoja na mwenyeji wao ambaye ni Mtanzania aitwaye  Salum Rashid (29) Mkazi wa Igomelo Manispaa ya Kahama Mkoa wa Shinyanga. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Mei 21,2021 majira ya saa 4:00 usiku katika mtaa wa Igomelo Manispaa ya Kahama wakiwa na mwenyeji wao huyo.

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia msako mkali unaondelea kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga wa kupambana na uhalifu na kwamba taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja tabia za kupokea na kuwahifadhi raia wa kigeni kwenye maeneo yao kwa sababu yoyote ile kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Peter Matiko (36),Mkazi wa Nyakato Mwanza  baada ya kukamatwa akiwa na madawa ya kulevya aina ya Mirungi bunda 50 yenye uzito wa Kg 25.

"Mtuhumiwa huyo alikamatwa mnamo tarehe 21.05.2021 majira ya saa 04:06 asubuhi huko maeneo ya Mtaa na Kata ya Ibinzamata ndani ya Manispaa  ya Shinyanga baada ya kutiliwa mashaka na askari waliokuwa doria maeneo hayo ambapo alikamatwa na alipopekuliwa alikutwa na madawa hayo ya kulevya aina ya Mirungi aliyokuwa ameyafunga katika vipande vya gazeti na kuweka katika mabegi mawili meusi aliyokuwa ameyabeba",ameeleza. 

Amesema Mtuhumiwa ni mtumiaji na pia muuzaji wa madawa hayo. Taratibu  za kumfikisha mahakamani zinaendelea.

Pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Masunga Nindwa (36), Mkazi wa Lunzewe Mkoani Geita baada ya kukamatwa akiwa na bhangi debe mbili sawa na uzito wa Kg 20.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa mnamo tarehe 21.05.2021 majira ya saa 04:49 usiku huko katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Kalunde iliyopo mtaa wa Agape kata ya Nyasubi Manispaa ya Kahama

"Pia tunamshikilia Elida Zacharia (19) ,Mkazi wa Kagongwa Kahama baada ya kukamatwa akiwa na bhangi  kete 111. Mtuhumiwa huyo alikamatwa mnamo tarehe 20.05.2021 majira ya saa 18:00 jioni huko mtaa wa Iponya kata ya Kagongwa nyumbani kwa Lucia Luhende Mama Bonge  ambaye ndiye mmliki wa nyumba na bangi hiyo",ameongeza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post