Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT.ABBASI AZITAKA SPORTS BETTING KUWA SEHEMU YA KUKUZA MICHEZO


Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi  amezitaka Kampuni za Ubashiri wa Michezo (Sports Betting) kuwa sehemu ya kuinua na  kukuza  michezo nchini.

Dkt. Abbasi  ameyasema hayo Mei 05, 2021 Jijini Dar es Salaam katika  kikao  na Kampuni hizo ambapo amesema kuwa  Michezo ya Kubashiri ( Sports Betting) inayo nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo  ya timu  za Taifa  hasa pale zinapokuwa katika mashindano.

“Lengo la Serikali kwa sasa ni kuwekeza kimkakati kwenye michezo, tuwe na mpango wa moja kwa moja wa kuzisaidia timu zetu za Taifa kifedha, mimi naamini tukishirikiana kwa karibu tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo.” Alisema Dkt. Abbasi.

Katibu Mkuu Dkt.Abbasi amesisitiza  kuwa  changamoto zilizopo katika Kampuni hizo zitatafutiwa ufumbuzi kupitia vikao  na njia mbalimbali baina ya Serikali na Kampuni hizo, ambapo amesisitiza  ushirikiano kwa pande hizo mbili katika kusaidia nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Ubashiri wa Michezo Tanzania (TSBA) Jimmy Kenneth ameiomba Serikali kutatua  baadhi ya changamoto ikiwemo  uwepo kwa kampuni za ubashiri ambazo hazina usajili nchini ambazo  zinaisababishia nchi kukosa mapato ambapo Dkt.Abbasi ameahidi kufanyia kazi suala hilo.

Naye Mwakilishi kutoka Biko Sports Goodhope Heaven alimshukuru Dkt. Abbasi kwa kuweza kukutana nao na kumshukuru kwa namna alivyoonesha moyo wa kusaidia Sekta ya Michezo nchini pamoja na  kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zao.

Wadau hao kwa pamoja wameonesha utayari wa kuzisaidia timu  za Taifa huku wakiiomba Serikali kuweka msisitizo wa  mazingira rafiki ya ulipaji kodi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com