Na Mwandishi Wetu, Dar es Salam
Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali imejipanga kuisaidia Timu ya Taifa kwa kuipatia fedha ili kuongeza ufanisi wa timu hiyo ndani na nje ya nchi.
Dkt. Abbasi amesema hayo Mei 3, 2021 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw.Alfred Kidau ambapo wamezungumzia namna ya kuiwezesha Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye maandalizi ya michuano ya awali ya kufunzu Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwezi Juni hadi Agosti 2021.
“Ili kupata matokeo mazuri wachezaji wetu lazima wawe vizuri kifedha hii itawasaidia kisaikolojia kuweza kupata matokeo mazuri.” Alisema Dkt. Abbasi.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuanzisha vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya michezo ikiwemo kurudisha mchezo wa Bahati Nasibu ((Sport Betting Nationary Lottary).
Kwa upande wake Bw. Alfread Kidau amesema maandalizi yote yamekamilika huku akieleza kuwa changamoto iliyobaki ni ukosefu wa rasilimali fedha ambapo ameshukuru namna Serikali inavyojipanga kukabili changamoto hiyo ikiwemo kusaidia posho za wanamichezo kutolewa mapema.
Kikao hicho pia Kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania Bw. Yusuph Singo.
Social Plugin